Ofisi ya Bunge yag’ang’aniwa

Muktasari:

Hilo ni moja ya mapendekezo yaliyotolewa na Bodi ya Wakurugenzi ya PPRA, baada ya taasisi hizo kukaguliwa na kuonyesha uwapo wa viashiria vya rushwa wakati wa utekelezaji wa ununuzi ya umma.

Dar es Salaam. Licha ya kuokoa Sh6 bilioni, Ofisi ya Bunge la Muungano ni miongoni mwa taasisi tisa ambazo Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imependekeza zichunguzwe na Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru) baada ya kuonyesha viashiria vya rushwa.

Hilo ni moja ya mapendekezo yaliyotolewa na Bodi ya Wakurugenzi ya PPRA, baada ya taasisi hizo kukaguliwa na kuonyesha uwapo wa viashiria vya rushwa wakati wa utekelezaji wa ununuzi ya umma.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA, Balozi Marten Lumbanga alisema baada ya kufanya ukaguzi na kubaini dosari kadhaa wamependekeza hatua mbalimbali zichukuliwe.

Vilevile, Bodi imependekeza hatua za nidhamu kuchukuliwa dhidi ya watumishi waliohusika kwenye miradi 15 iliyopata alama mbaya kwenye ukaguzi wa kupima thamani halisi ya fedha.