Ojadact yataka uchunguzi kupotea kwa Mwandishi wa Mwananchi

KUTOWEKA KWA AZORI GWANDA KWAWASHITUA WAANDISHI WENZAKE

Muktasari:

Gwanda ambaye kituo chake cha kazi ni Pwani ametoweka katika mazingira ya kutatanisha tangu Novemba 21 na mpaka sasa hajulikani alipo.

Mwanza. Chama cha Waandishi wa Habari wa Kupinga Vita Matumizi Dawa za Kulevya na Uhalifu (Ojadact), kimevitaka vyombo vya dola na mamlaka nyingine serikalini kumtafuta na kumpata mwandishi wa kujitegemea wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Azory Gwanda.

Gwanda ambaye kituo chake cha kazi ni Pwani ametoweka katika mazingira ya kutatanisha tangu Novemba 21 na mpaka sasa hajulikani alipo.

Mbali ya Ojadact, vyombo vya habari vya kimataifa na wadau mbalimbali wa habari wamezungumzia kutoweka kwa Gwanda wakitaka juhudi za makusudi za kutafutwa na kupatikana kwa mwandishi huyo.

Akizungumza na mwaandishi wa habari jijini hapa jana, Mwenyekiti wa Ojadact, Edwine Soko aliwaomba wadau wa habari nchini kuunganisha nguvu katika kumtafuta na kuvishinikiza vyombo na mamlaka husika kumtafuta mwandishi huyo.

“Hatuwezi kuendelea kuvumilia tabia inayoanza kuzoeleka nchini ya watu kupotea bila kujulikana walipo huku vyombo vya dola vyenye dhamana ya ulinzi na usalama wa raia vikichukulia kawaida, kama jamii lazima tusema hapana kwa sababu huo siyo aina ya Utanzania tuliouzoea,” alisema Soko.

Soko alisema jamii haipaswi kuendelea kufumbia macho vitendo vya watu kupotea na wengine miili yao kuokotwa katika fukwe za bahari na mito nchini kwa sababu vinakiuka Ibara ya 14 ya Katiba inayolinda haki ya kuishi kwa kila mtu.

Alisema tukio la Gwanda lina dalili zote za uovu kwa sababu muda ambao hajaonekana unazidi hata ule unaoruhusiwa mtuhumiwa kushikiliwa kisheria hata na vyombo vya dola kabla ya kumfikisha mahakamani.

Kwa mujibu wa mkewe, Anna Pinon (35), Novemba 21, Agwanda aliaga nyumbani kwake Kibiti kuwa kuwa anaenda kazini lakini hakufika wala kurejea nyumbani.

Mmoja wa waandishi wa habari jijini Mwanza, Halima Juma alisema kitendo cha Gwanda kupotea kimeibua hofu miongoni mwa waandishi wa habari nchini, hasa wanaofuatilia na kuibua habari zinazopiga vita uovu, ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka kwa watu wenye uwezo na mamlaka.

Kupitia kurasa zake za kujamii, mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe aliandika ‘’Maswali kwa @MwananchiNews 1) alikuwa ana ‘assignment’ yeyote kutoka kwenu alipotekwa huko Kibiti? 2) kama ndio kwanini hamsemi hilo? 3) Mna Habari yake yeyote hamjaichapisha gazetini?

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kilisema ‘’tunaungana na uongozi wa @MwananchiNews kutoa wito kwa Jeshi la Polisi Tanzania…kuchukua hatua ili ndugu Azory Gwanda aweze kupatikana. #MrudisheniAzoryGwanda.”

Vituo vya habari za kimataifa vya Fox News, New York Times, Daily Nation walizungumzia kupotea kwa mwandishi Gwanda.