Oktoba Mosi yawa dili, yaanza kugombewa

Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum akishiriki kufanya usafi na askari wa JWTZ katika kambi ya Lugalo Dar es Salam jana ikiwa ni maadhimisho ya miaka 52 ya jeshi hilo. Picha na Emmanueli Herman

Muktasari:

Na ili kufanikisha uzinduzi huo, Jeshi la Wananchi (JWTZ) limeombwa kushiriki huku mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam akizuia mikutano yoyote ambayo itaonekana haina tija.

Dar es Salam. Ni matukio mawili tu kati ya manne yaliyofanyika jana baada ya Chadema kuahirisha kwa siku 30 maandamano na mikutano yake kote nchini, lakini Oktoba Mosi ambayo chama hicho kimepanga kuendesha shughuli hizo, sasa itakumbana na uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti jijini Dar es Salaam.

Na ili kufanikisha uzinduzi huo, Jeshi la Wananchi (JWTZ) limeombwa kushiriki huku mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam akizuia mikutano yoyote ambayo itaonekana haina tija.

Chadema ilikuwa imepanga kuzindua operesheni iliyoibatiza jina la Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta), kwa kufanya mikutano na maandamano kote nchini, lakini ikatangaza kuahirisha juzi ikieleza kuwa imezingatia ushauri kutoka kwa viongozi wa dini, taasisi na watu mashuhuri.

Siku ya jana, pia ilikuwa na tukio la kihistoria la kupatwa kwa jua ambalo lilivuta watu kutoka kila kona ya dunia kutokana na tukio hilo kuonekana vizuri zaidi kusini mwa nchi.

Matukio mengine ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuhamia Dodoma, Jeshi la Wananchi kuadhimisha miaka 52 tangu lianzishwe kwa kufanya shughuli za usafi kote nchini na viongozi wa Chadema kutakiwa kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi.

Lakini matukio mawili tu yalifanyika; kupatwa kwa jua na maadhimisho ya JWTZ ambayo ilifanya shughuli zake kwenye kambi mbili za Lugalo na Airwing, tofauti na ilivyoeleza kuwa kungekuwepo na mazoezi mitaani, huku ndege za kivita zikipita angani jijini Dar es Salaam.

Wakati Chadema ikiwa imeahirisha maandamano na mikutano hadi Oktoba Mosi kutoa muda kwa viongozi wa dini kukutana na Rais John Magufuli kujadili suluhu ya madai yao, mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amepanga siku hiyo kuwa ni ya uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti.

“Nimezungumza na watu wa hali ya hewa, wameniambia tukianza mapema miti hii haitakufa. Siku ya Oktoba Mosi kila mtu atakuwa na mti wake, tutawaarifu kupitia wakuu wa wilaya miti itapatikana wapi baada ya taratibu zake kukamilika,” alisema Makonda mbele ya Rais Magufuli kwenye mkutano wa 14 wa wahandisi kwenye ukumbi wa Mlimani City.

Makonda alisema siku hiyo vikosi vya ulinzi na usalama vitashiriki kupanda miti na kumuomba Rais amsaidie na amvumilie ili atende kazi yake ya kuhakikisha mkoa wa Dar es Salaam unakuwa na amani sambamba na kufanikisha kutekeleza mpango huo wa upandaji miti.

“Watakaopewa kibali ni wale wanaojadili maendeleo, lakini si wapigakelele. Mikutano kama hii (ya wahandisi) inayojadili masuala muhimu kabisa kwa maendeleo ya nchi, itaruhusiwa bila shaka yoyote.”

Makonda alisema kampeni hiyo itawahusisha pia wananchi, viongozi wa dini na kamati nzima ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Dar es Salaam na kwamba jumla ya miti milioni 4 inatarajiwa kupandwa siku hiyo.

Alisema ameamua kushirikisha vyombo vya ulinzi na usalama kwa sababu ni watiifu na wazalendo kwa Taifa wakati kada nyingine zimejielekeza kwenye siasa.

Hata hivyo, Rais hakuzungumzia maombi hayo zaidi ya kusema kuwa Makonda naye amekuwa mhandisi kutokana na kutoa maelekezo.

Kabla ya Makonda kutangaza Oktoba Mosi kuwa siku ya kupanda miti, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema wamekutana na viongozi wa dini zaidi ya mara moja kwa ajili ya kupata maoni na ushauri kuhusu maandamano yao, ambayo Jeshi la Polisi liliyapiga marufuku kwa maelezo kuwa yalikuwa na viashiria vya kuvunja amani.

Baadaye JWTZ ilisema ingeadhimisha kuzaliwa kwa jeshi hilo kwa askari wake kufanya mazoezi na kuonyesha silaha zao za angani na nchi kavu, kufanya usafi mitaani na kujitolea damu, huku likibainisha kuwa linaamini hakungekuwa na maandamano yoyote kwa kuwa yameshazuiwa.

Shughuli ya Waziri Mkuu kuhamia Dodoma ilishatangazwa juzi kuwa imeahirishwa hadi baada ya Bunge la Septemba, wakati Lowassa na viongozi wengine wa Chadema waliotakiwa kuripoti polisi jana, hawakufanya hivyo.

Wakati Chadema ikiwa imesitisha kwa muda maandamano na mikutano kupisha majadiliano, Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) umesema kuwa hakutakuwa na mazungumzo, majadiliano wala mijadala kati ya Serikali, CCM na chama hicho kikuu cha upinzani.

Badala yake, umoja huo umemuomba Rais Magufuli kuendelea kuimarisha maendeleo ya uchumi na juhudi za kuiletea nchi mabadiliko ili kupambana na umasikini, ujinga na maradhi.

Umoja huo umedai kuwa kitendo cha Chadema kuahirisha maandamano na mikutano hiyo, ni usaliti na utapeli wa kisiasa na kwamba sababu walizotoa kuahirisha mpango huo ni visingizio vya hadaa, ghiliba na uzushi.

Kaimu Katibu Mkuu wa umoja huo, Shaka Hamdu Shaka alisema UVCCM, ambayo pia ilitangaza kufanya maandamano Agosti 31 kabla ya kuyaahirisha siku moja kabla, ilikuwa inajua mapema kwamba Chadema na viongozi wake walikuwa wakifanya maigizo katika siasa kwa kuwa hawana nguvu wala jeuri ya kuandamana kwa mustakabari wa nchi.

Katibu huyo alisema wafuasi wa chama hicho wameshindwa kuandamana Septemba Mosi na hawataweza Oktoba Mosi, akidai wameona kilichotaka kufanyika ni utapeli wa kisiasa.

Alisema UVCCM imeshangazwa na madai yaliyotolewa na chama hicho kwamba wamekuwa wakikutana na viongozi wa dini na mashirika ya kiraia, kisheria ambao wamewataka wasitishe maandamano yao kwa muda hadi Oktoba Mosi.

“Je, hapo awali chama kilishirikiana na vongozi hao katika kupanga na kuitisha maandaano hayo yenye lengo la kumdhihaki Rais na kumuita kiongozi aliyechaguliwa kikatiba na kisheria kwamba ni dikteta?” alihoji.

Alisema kila mtu anafahamu baada ya Rais Magufuli kuchaguliwa Serikali yake imekuwa ikihimiza dhana ya kuimarisha uwajibikaji, utendaji wenye ufanisi na tija, kuwepo nidhamu ya kazi, kupiga vita ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma lakini pia kukusanya kodi na kuongeza mapato ya Taifa.

“Wanachotaka (Chadema) ni kuendeleza siasa za mitaani, maandamano yasiyo na umuhimu, malumbano na mabishano badala ya kuwahimiza wananchi wafanyabiashara, wafanyakazi, wavuvi na wakulima wafanye kazi kwa bidii, wajitume wazalishe mali ili kujenga Taifa.

JWTZ walivyoadhimisha miaka 52

Katika kuadhimisha miaka 52 ya JWTZ, Makonda alishiriki kufanya usafi na askari hao katika kambi ya Lugalo iliyopo wilayani Kinondoni.

Makonda aliambatana na kamati ya amani ya viongozi wa dini wa Dar es Salaam, ikiongozwa na mwenyekiti wake Alhadi Mussa Salum.

Makonda aliitaja barabara ya Mwenge –Ubungo kuwa ni miongoni mwa barabara zitakazopandwa miti siku hiyo na watashirikiana na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).

Mkuu wa Brigedia ya Mashariki, Brigedia Jenerali Sharif Othmani alisema JWTZ imekuwa bega kwa bega na wananchi ikiamini kuwa haiwezi kufanya kazi bila kushirikiana nao kwa ukaribu.

“Nawaomba wananchi waelewe kuwa JWTZ ni kama samaki na wananchi ni kama maji, hivyo sisi tunategemea sana maji. Ukimtoa samaki kwenye maji hawezi kuishi. Kwa hiyo tunaomba ushirikiano wa hali ya juu, hili sio jeshi la Tanzania, ni jeshi la wananchi wa Tanzania,” alisema.

Sheikh Salum alisema wao kama viongozi wa dini watashiriki kikamilifu siku ya Oktoba Mosi kupanda miti.

Katika maeneo mengine ya jiji, magari ya polisi, ambayo katika siku za kuelekea Septemba Mosi yalikuwa yakizunguka mitaani yakiwa yamejaa polisi wenye silaha, jana yalionekana yakirandaranda na mengine kuegeshwa, huku polisi wakionekana katika maeneo machache.

Katika Manispaa ya Ilala, Mwananchi haikuona shughuli za usafi iliyokuwa ikifanyika, badala yake watu walikuwa wakiendelea na shughuli zao za kila siku.

Katika maeneo ya vituo vya pikipiki za abiria na yale yenye watu wengi kama Kariakoo, Msimbazi, Posta na Ferry, watu waliendelea na shughuli zao kama kawaida huku polisi waliobeba bunduki na mabomu ya machozi wakirandaranda.

Katika maeneo ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Hospitali ya Amana na Ocean Road hakukuwa na shughuli yoyote ya usafi.

Wilayani Temeke, jeshi hilo lilifanya usafi maeneo ya Hospitali ya Rufaa ya Temeke na Soko la Stereo siku tatu kabla ya jana.

“Walifanya usafi hapa tuliwaona na ni jambo zuri kwamba wameanza kuonyesha umuhimu wa usafi na sisi tutawaunga mkono kwa kuiga walichofanya,” alisema mfanyabiashara mmoja sokoni hapo aliyejitambulisha kwa jina la Juma.

Polisi walionekana wakifanya doria katika maeneo ya Mwembeyanga, ambako gari la polisi liliegeshwa kwa muda mrefu, Temeke Mwisho, Mtoni Kwa Azizi Ali na Mbagala.

Mkoani Arusha, askari wa JWTZ walijitokeza kwenye kambi mbalimbali kuchangia damu, kutoa misaada kwa walemavu na kufanya usafi.

Mkuu wa shule ya mafunzo ya vifaru ya kambi ya Sokoine wilayani Monduli, Brigedia Jenerali Rajabu Hanti na Mkuu wa Chuo cha Jeshi cha Monduli(TMA), Meja Jenerali Peter Masao waliwaambia waandishi wa habari kuwa utoaji damu na kufanya usafi ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 52.

Brigedia Jenerali Hanti alikuwa na wanajeshi Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru ambako walifanya usafi na kuchangia damu na kutoa wito kwa watu wengine kujitokeza.

Naye Meja Jenerali Masao aliongoza maafisa wa jeshi hilo kutoa huduma ya upimaji afya, kutoa misaada kwa kituo cha walemavu Monduli, kufanya usafi Hospitali ya Monduli na kushiriki michezo mbali mbali na wananchi.