Thursday, August 16, 2018

Ole Nasha ampa mkandarasi wiki mbili

 

By Haika Kimaro, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Mtwara. Naibu Waziri wa Elimu,  Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha ametoa wiki mbili kwa mkandarasi anayefanya ukarabati wa majengo katika shule ya sekondari ya Mtwara Ufundi kuhakikisha anayakabidhi.

Ametoa kauli hiyo jana Agosti 15, 2018 katika ziara yake ya kikazi ya kukagua miundombinu ya shule.

“Lazima waje ndani ya wiki mbili wakabidhi mradi na wasipofanya hivyo hakutakuwa na muda wa kutazama na kueleza upungufu,” amesema.

“Majengo yakishaanza kutumika itakuwa vigumu kujua  kama ni wao hawajafanya vizuri au kuna uharibifu umefanyika.”

Naibu waziri huyo pia alikutana na viongozi wa sekta ya elimu na wakuu wa shule na kufanya nao mazungumzo.

Katika mazungumzo hayo alielezwa siri ya Mkoa wa Mtwara kufanya vizuri katika matokeo ya kidato cha sita, kuombwa yafanyike mabadiliko ya utungaji wa mtihani wa darasa la saba.

Mwalimu Mkuu wa sekondari ya Nangwanda, Beatrice Marwa ameshauri Serikali kubadili aina ya mtihani wa kumaliza darasa la saba ili kubaini watoto wanaofaulu na kuanza kidato cha kwanza wakiwa hawajui kusoma na kuandika.

“Naomba kutoa ushauri kwa upande wa shule za msingi, mtihani wa kuhitimu darasa la saba mfumo wake ubadilike turudishe wa zamani wa swali, kazi na jibu,” amesema.

“Kama ni hesabu ionekana anafanya hesabu na anaandika mwenye jibu, hii itasaidia kubaini watoto wasiojua kusoma na kuandika kuliko hii ya kuchagua mtoto anaweza akabahatisha na kufaulu. Akifika sekondari unagundua hajiwezi katika kuandika.”

 Ole Nasha ameahidi kulifanyia kazi wazo hilo kwani tayari lipo na mipango imeshaanza.

 

-->