Bunge kumhoji Ole Sendeka

Muktasari:

Ni kwa sauti inayodaiwa kuwa yake akilizungumzia Bunge

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka anatakiwa kujitetea mbele ya Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka kuhusu kauli zake zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kwa kile kinachodaiwa kuwa zinakejeli na kudharau Bunge.

Taarifa kutoka Ofisi ya Spika wa Bunge iliyotolewa leo Jumanne inaeleza kuwa Spika Job Ndugai ametoa maelekezo kwa kamati hiyo kumchunguza mbunge huyo wa zamani wa jimbo la Simanjiro.

Katika taarifa hiyo inaelezwa kuwa Spika amechukua hatua hiyo kufuatia kauli zinazonukuliwa katika mitandao ya kijamii kwa lugha za kimasai, kiswahili na kiingereza  zikiashiria kejeli na dharau kwa Bunge.

Spika ameitaka kamati hiyo kumuita mkuu huyo wa mkoa, kumhoji na kubaini ukweli na dhamira  ya kauli hizo na kutoa mapendekezo kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa na Bunge.