Ole wenu, bodaboda Kilosa waonywa

Muktasari:

Onyo hilo limetolewa na Mkuu wa wilaya hiyo, Adam Mgoyi aliyesema vyombo vya dola havitamuachia mtu au kikundi kitakachojichukulia sheria mkononi kwa kisingizo cha migogoro ya wakulima na wafugaji.

Morogoro. Serikali imewaonya madereva wa bodaboda wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro kuacha kujichukulia sheria mikononi kwa kuwapiga watu bila sababu za msingi.

Onyo hilo limetolewa na Mkuu wa wilaya hiyo, Adam Mgoyi aliyesema vyombo vya dola havitamuachia mtu au kikundi kitakachojichukulia sheria mkononi kwa kisingizo cha migogoro ya wakulima na wafugaji.

Mgoyi ameoa onyo hilo wakati akizungumza na wakazi wa Mji wa Mikumi kuhusu kitendo cha waendesha bodaboda kuingia mitaani na kuwapiga wafugaji.

Amewaonya wakazi hao kuacha kujiingiza kwenye vurugu au uchochezi badala yake waviachie vyombo vya dola vifanye kazi yake.

Bodaboda hao walikuwa wakiwatuhumu wafugaji kuhusika na mauaji ya mwenzao, Joseph Msimbe.

Mkuu huyo amesema kwa mujibu wa sheria yeye ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, hivyo hawezi kukubali kuona amani inatoweka kwa ajili ya mtu au kikundi chochote.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei amesema kuwa mauaji hayo hayanahusiani na migogoro ya wakulima na wafugaji.

Matei amesema katika vurugu hizo, watu sita wamekamatwa huku watatu jamii ya wafugaji wakijeruhiwa kwa kupigwa na marungu na kulazwa Hospitali ya Mtakatifu Kizito Mikumi kwa matibabu.