Pacha waliotenganishwa waendelea vizuri MNH

Muktasari:

  • Pacha hao ambao walifanyiwa upasuaji Septemba 22 mwaka huu uliohusisha jopo la madaktari bingwa 10 wa upasuaji wa watoto wanaendelea vizuri

Dar es Salaam. Pacha waliofanyiwa upasuaji kutenganishwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wanaendelea vizuri.

Kulwa na Doto Michael walizaliwa Julai 12 kwa njia ya kawaida katika kijiji cha Vigwaza mkoani Pwani, wakiwa wameungana sehemu ya tumbo.

Upasuaji wa watoto hao ambao wote na wavulana ulifanyika Septemba 22 mwaka huu ukihusisha jopo la madaktari bingwa wa upasuaji 10.

Akazungumza na Mwananchi leo Jumatatu Oktoba Mosi 2018, Ofisa Uhusiano Msaidizi MNH, John Steven amesema afya za pacha hao zitaendelea kuimarika kama ilivyo hivi sasa huenda wakaruhusiwa muda wowote.

“Kwa sasa wananyonya vizuri, wanaendelea na dawa zao hata kwa upande wa mama yao naye afya yake ipo salama,” amesema.

Kwa upande wake mama mzazi wa pacha hao Ester Simoni amewaomba Watanzania waendelee kuwaombea ili waweze kuruhusiwa hospitalini hapo.

“Nashukuru Mungu kwa kweli hivi sasa wanaendelea vizuri wala hawasumbui hata vidonda vimeshaanza kukauka na daktari alisema tutaruhusiwa baada ya wiki mbili hivyo naomba Watanzania wazidi kutuombea,”amesema Ester.