Pacha walioungana Maria na Consolata kuchunguzwa nje ya nchi

Muktasari:

  • Pacha hao wanaosoma Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha (Rucu) mkoani Iringa, wanaendelea kupatiwa matibabu ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam.

Pacha walioungana Maria na Consolata Mwakikuti wamesema wakati wowote wataenda Afrika Kusini kwa uchunguzi zaidi wa afya zao.

Pacha hao wanaosoma Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha (Rucu) mkoani Iringa, wanaendelea kupatiwa matibabu ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam.

Maria na Consolata walifikishwa JKCI wakitokea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa walikokuwa wamelazwa tangu Desemba 28 mwaka jana.

Katika ujumbe walioutuma juzi jioni pacha hao walisema wanahitaji maombi zaidi wakati huu wanapotarajia kufanyiwa uchunguzi Afrika Kusini.

“Jamani ni sisi Maria na Consolata tunaomba sala zenu maana tunatarajia kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya uchunguzi zaidi ila kwa sasa tuko Dar es Salaam. Tarehe tutajuzana. Tunahitaji sala zenu,” unasomeka ujumbe wa pacha hao waliozungumza na mwandishi wa Mwananchi.

Ofisa Uhusiano wa JKCI, Mulid Kikondo akizungumza na Mwananchi jana alisema kulikuwa na majadiliano kuhusu kuwapeleka pacha hao nje ya nchi kwa uchunguzi zaidi lakini bado hawajafikia muafaka.

“Kama unavyojua ni wawili kwa hiyo kinachotokea ni kwamba huyu anapopata nafuu mwingine anakuwa anaumwa, tulijadili suala hilo bado muafaka haujafikiwa,” alisema Kikondo.

Pacha hao wapo chini ya uangalizi wa jopo la madaktari bingwa wakiongozwa na Mkurugenzi wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi.

Wawili hao wameonyesha uwezo wa kielimu tangu walipohitimu na kufaulu darasa la saba mwaka 2010 katika Shule ya Msingi ya Ikonda wilayani Makete na badaye kidato cha nne katika shule ya Sekondari ya Udzungwa wilayani Kilolo.

Maria na Consolata wanalelewa na Serikali ikishirikiana na Rucu.

Awali Shirika la Masista la Maria Consolata liliwalea na kuwasomesha tangu walipozaliwa hadi walipohitimu kidato cha sita mwaka jana.

Ni watoto yatima waliozaliwa katika Hospitali ya Misheni ya Ikonda wilayani Makete mkoani Njombe mwaka 1996.