Pacha walioungana watimiza ndoto yao, watinga chuo kikuu

Muktasari:

Ndoto hiyo sasa imetimia baada ya kuripoti katika Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki Ruaha (Rucu) tayari kwa kuanza masomo ya shahada ya kwanza.

Iringa. Kuanza masomo ya chuo kikuu ilikuwa ndoto kubwa ya pacha walioungana Maria na Consolata Mwakikuti tangu wakiwa darasa la saba.

Ndoto hiyo sasa imetimia baada ya kuripoti katika Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki Ruaha (Rucu) tayari kwa kuanza masomo ya shahada ya kwanza.

Katika matokeo ya kidato cha sita, pacha hao walifaulu mtihani wao wakipata daraja la pili (division two) hivyo kuwa na mwendelezo mzuri wa ufaulu kama ilivyokuwa wakiwa darasa la saba na kidato cha nne.

Wakizungumza na mwandishi wetu jana huku kila kila mmoja akidakia anachoongea mwenzake, pacha hao walielezea furaha yao huku wakiushukuru uongozi wa chuo hicho na wanafunzi kutokana na jinsi walivyopokewa na kuandaliwa mazingira mazuri ya kusomea na kuishi.

Maria alisema wamewasili mapema chuoni kwa sababu wanataka kujifunza kompyuta ili waendane na kasi ya wanafunzi wengine.

Alisema wanalishukuru Shirika la Wamisionari la Masista wa Consolata kwa kuwalea tangu wakiwa wadogo na kuwapa moyo pamoja na wafadhili mbalimbali waliowasaidia hadi kutimiza ndoto yao ya kufika chuo kikuu.

Sista Jane Lugi wa Shirika la Consolata alisema wamepeleka pacha hao chuoni mapema ili wajifunze kompyuta, somo ambalo litawasaidia katika masomo yao.

“Sisi tuliwatunza tukiwa Kilolo, hapa watatunzwa na masista wa Teresia ambao wamewaandalia mazingira mazuri ya kuishi kama walivyoomba, tumeridhika na tunawatakia kila la heri. Tutakuwa tunakuja kuwaona mara kwa mara,” alisema Sista Jane.

Pacha hao wameandaliwa vyumba vitatu, jiko, sebule na maliwato inayojitegemea ndani ya chumba chao.

Akizungumzia ujio wa wanafunzi hao, Makamu Mkuu wa Chuo (Fedha na Utawala), Padri Kelvin Haule alisema, “Tunaona fahari pacha hawa kutuamini na wanaweza kuishi vizuri na kuendelea kutimiza ndoto yao na hatimaye kuhitimu chuo. Tumewapokea mapema ili wajifunze kompyuta kama walivyoomba.”

Padri Haule alisema wanafunzi hao waliozaliwa mnamo mwaka 1996, wataanza kujifunza kompyuta leo kabla ya kuungana na wenzao katika muhula wa kwanza wa masomo unaotarajiwa kuanza mwezi ujao.

Kuhusu kozi hiyo, mwalimu wa kompyuta katika chuo hicho, Robert Manase alihidi kwamba atahakikisha anawasaidia kuendana na kasi pamoja na kulijua somo hilo.

“Maria na Consolata wanafahamu kidogo kompyuta lakini ni kutokana na mazingira.”

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Maria Consolata, walikohitimu kidato cha nne, Jefred Kipingi alisema hatua waliyofikia pacha hao inatia moyo.

Maria na Consolata walihitimu darasa la saba katika Shule ya Msingi Ikonda wilayani Makete na baadaye kujiunga na shule ya Sekondari ya Maria Consolata kabla ya kuhitimu kidato cha sita katika shule ya Udzungwa wilayani Makete.

Shirika la Maria Consolata ndilo lililowalea pacha hao tangu wakiwa wadogo baada ya kufiwa na wazazi wao wote wawili.

Baba yao Alfred Mwakikuti alifariki dunia wakiwa na umri wa miaka mitatu wakati mama yao aliwaacha wakiwa bado wachanga.