Pancho Latino kuzikwa Jumamosi, kuagwa kesho

Joshua Magawa maarufu Pancho Latino

Muktasari:

Mwili wa  mtayarishaji huyo wa muziki utasafirishwa kesho Oktoba 12, 2018 baada ya kuagwa katika Hospitali ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Shughuli za kuaga mwili wa mtayarishaji muziki nchini Joshua Magawa maarufu Pancho Latino zinatarajiwa kufanyika kesho Hospitali ya Lugalo, jijini Dar es Salaam na atazikwa Jumamosi nyumbani kwao Gairo, mkoani Morogoro.

Pancho alifariki juzi akiwa njiani kuwahishwa hospitali baada ya kuokolewa akizama majini katika kisiwa cha Mbudya alipokuwa akiogelea.

Msemaji wa kamati ya mazishi, rapa Fid Q amesema shughuli hizo zitaanza saa 4:00 asubuhi na baada ya hapo mwili utasafirishwa kwenda kwao wilayani Gairo mkoani Morogoro ambapo wanatarajia kuingia usiku.

Kuhusu mazishi msemaji huyo ambaye ni msanii wa Bongo Fleva, amesema wanatarajia kuzika siku ya Jumamosi.

Enzi za uhai wake, Pancho alijizolea umaarufu kwa kutengeneza nyimbo mbalimbali ikiwemo wa Chid Benz, Dar es Salaam Stand Up, Baby Candy wa Dully Sykes, Closer wa Vanessa na nyinginezo nyingi.

Pancho aliyezaliwa Mei 5, 1988 ni mtoto wa mwisho kati ya watoto tisa katika familia ya Mzee Joshua Magawa.