Panya watafuna fedha ATM

Assam, India. Panya wamefanya uharibifu mkubwa kwenye mashine ya kutolea fedha iliyopo kwenye benki moja katika Jimbo la Assam nchini India.

 

Mafundi waliokuwa wanatengeneza mashine hiyo ya ATM, walipigwa na butwaa baada ya kuona vipande vya fedha vikiwa vimetapakaa ndani ya mashine hiyo.

 

Noti zenye thamani ya rupia 1.2m (zaidi ya Sh35 milioni) zilikuwa zimechanwa na kuraruliwa na panya katika benki mashine hiyo.

 

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Utangazaji la Uingereza (BBC), Polisi wanasema panya hao pengine waliiingia ndani ya mtambo huo kwa kupitia kwenye tundu lililokuwa litumiwe kuingizia nyaya.

 

BBC waliendelea kunukuu taarifa za gazeti la Hindustan Times lililodai kwamba picha zinazoonyesha pesa zilizokuwa zimetafunwa na panya hao katika mtambo huo wa benki zimesambazwa kwenye mtandao wa Twitter.

 

Moja ya picha hizo inaonyesha mzoga wa panya hao kwenye mabaki ya noti hizo.

 

Ofisa wa polisi Prakash Sonowal alisema kwamba mtambo huo umekuwa haufanyi kazi kwa siku 12.