Papa Francis asema hakuna jehanamu

Muktasari:

Akizungumza Alhamisi katika mahojiano na gazeti la La Republica Papa Francis (81) alisema baada ya kifo, roho za watu ambao wanatubu zitapata msamaha kutoka kwa Mungu na kujiunga na zingatio la tafakari ya Mwenyezi Mungu


Roma, Italia. Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amenukuliwa akisema hakuna jehanamu ambako roho za wenye dhambi zitaadhibiwa milele.

Akizungumza Alhamisi katika mahojiano na gazeti la La Republica, Papa Francis (81) alisema baada ya kifo, roho za watu ambao wanatubu zitapata msamaha kutoka kwa Mungu na kujiunga na zingatio la tafakari ya Mwenyezi Mungu, lakini wale ambao hawatatubu hawatapata msamaha, watatoweka.

Francis aliongeza kwamba moto hakuna, kile kilichopo ni kutoweka kwa roho zenye dhambi.

Papa alihojiwa na mwandishi wa habari maarufu nchini Italia kabla ya Sikukuu ya Pasaka kuhusu imani na dini.

Baadaye Papa Francis alitekeleza kanuni ya kidini ya kuosha miguu inayofanyika kabla ya Sikukuu ya Pasaka ambapo alifanya hivyo katika gereza la Regina Coeli huku kukiwa na ulinzi mkali katika mji huo mkuu wa Italia.

Katika ibada hiyo Papa aliwahimiza wafungwa kutoacha matumaini yao yafunikwe kama mtoto wa jicho unavyofunika macho na akafichua kwamba yeye binafsi anasumbuliwa na hali kama hiyo na anatarajiwa kufanyiwa operesheni mwakani.

Francis, 81, alifichua habari hizo alipokuwa anaagana na maofisa wa Gereza la Regina Coeli ambako aliosha miguu ya wafungwa 12.

Miongoni mwa wafungwa 12 waliooshwa walikuwemo Wakatoliki, Waislamu, Waorthodox na Wabudha. Wafungwa hao ni kutoka Italia, Ufilipino, Morocco, Moldova, Colombia, Nigeria na Sierra Leone.