Uraia wa Canada ulivyomponza mshirika wa Odinga

Muktasari:

Alisema wakati Miguna alikamatwa, serikali ya Canada iliiandikia barua Kenya kuelezea wasiwasi kwamba raia wake alikuwa akisumbuliwa na walitaka kumrudisha.


Nairobi, Kenya. Mtu aliyejitangaza kuwa ni “jenerali” wa Vuguvugu la Kuikaidi Serikali (NRM), Miguna Miguna, Jumanne usiku 'amefukuzwa’ Kenya na kurejeshwa Canada.

Miguna alisafirishwa kwa ndege ya Shirika la KLM iliyotoka Nairobi saa 10:00 kasoro dakika kadhaa kwenda Amsterdam, Uholanzi, mwanasheria wake John Khaminwa alisema.

"Tumefahamishwa kwa uhakika kuwa Miguna Miguna amelazimishwa kuingia kwenye ndege ya KLM baada ya "kufukuzwa" akisafirishwa kwenda Canada. Sasa, unawezaje kumfukuza raia wa Kenya? Nchi hii imesimamiwa na wahalifu, "mwanasheria mwingine Nelson Havi aliandika juu ya Twitter.

Twitter rasmi ya chumba cha habari cha serikali ilisema,'' Miguna amerudishwa nyumbani. Mahakama iliamuru afunguliwe na waziri wa mambo ya ndani aliitii amri na hata ilimsaidia kwa kumpa tiketi ya kurudi nyumbani.”

 

Wizara ya Mambo ya Ndani inadai kwamba Miguna aliukana uraia wa Kenya miaka kadhaa ya nyuma. Msemaji Mwenda Njoka alisema mwanasheria huyo hakuwahi kujihangaisha kuomba upya.

"Miguna aliukana uraia wake wa Kenya miaka ya nyuma, alipata uraia wa Canada na hakuwahi kujihangaisha kuomba upya uraia wa Kenya kwa namna aliyotumia kisheria wala hakuwahi kusema kuwa alikuwa na uraia wa nchi nyingine licha ya kuwa mwanasheria ambaye angepaswa kujua zaidi," Mwenda alisema kupitia Twitter.

Akaunti hiyo iliongeza kuwa Miguna ''alihuisha pasipoti yake ya Canada Juni 16, 2017”.

Haikuweza kueleweka serikali ilitumia sheria gani kumfukuza Miguna kutoka Kenya kwani Katiba inamhakikishia uraia ikimtambua kuwa ni raia wa Kenya kwa kuzaliwa.

Ofisa wa ngazi ya juu wa serikali alisema kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani itatoa taarifa ya kina asubuhi.

Alisema wakati Miguna alikamatwa, serikali ya Canada iliiandikia barua Kenya kuelezea wasiwasi kwamba raia wake alikuwa akisumbuliwa na walitaka kumrudisha.

Jumanne iliyopita Miguna alielezea jinsi alivyokuwa ameshikiliwa kwa muda wa siku tano bila kupata fursa ya kuwasiliana na familia yake au mwanasheria baada ya kukamatwa Ijumaa iliyopita.

Alisema maofisa wa polisi walimdhihaki kwa kumfunga kwenye mazingira "yasiyofaa kuishi binadamu."

Miguna alikuwa akizungumza katika Mahakama ya Kajiado ambako alifikishwa baada ya kukamatwa Ijumaa iliyopita akituhumiwa kushiriki sherehe ambazo mpinzani mkuu Raila Odinga aliapa kuwa rais wa watu Januari 30.