Password inavyoweza kuokoa au kuangamiza maisha ya mtu

Muktasari:

  • Hata hivyo, baadhi hupendelea kuweka neno hilo la kufungulia simu kutokana na sababu mbalimbali, kubwa ikiwa usalama wa simu zao.

Dar es Salaam. Zipo simulizi kadhaa za baadhi ya watu waliofanikiwa kuokoa uhai wao au wa wapendwa wao kwa kutoweka nywila (password) kwenye simu zao za mkononi.

Hata hivyo, baadhi hupendelea kuweka neno hilo la kufungulia simu kutokana na sababu mbalimbali, kubwa ikiwa usalama wa simu zao.

Nywila inasaidia kufanya taarifa muhimu na za siri zilizomo kwenye simu zisiweze kufikiwa na mtu asiyeimiliki hadi kwa mtu anayeijua na hivyo huzuia watu wengine kutumia simu yako pindi inapoibiwa.

Baadhi ya watumiaji wa simu hizo na wachambuzi mbalimbali wanasema kuna uzuri na ubaya wa kuweka nywila kwenye simu.

Mmoja wa watumiaji wa simu, Nancy Nyalusi alisema tangu mdogo wake anayeitwa Hitra alipopata ajali mbaya ya barabarani na simu yake ambayo haikuwa na nywila, kutumika kutafuta ndugu zake, hajawahi tena kuweka neno la siri la kufungulia simu.

Alisema taarifa hiyo iliwafanya wawahi eneo la tukio kisha kumuwahisha hospitali kwa ajili ya matibabu.

Hitra alisema huwa hapendelei kuweka nywila kwenye simu yake hasa eneo la kupiga japo wakati akifanya hiyo, hakujua kama ipo siku itatumika kuokoa maisha yake.

Mkazi mwingine wa Magomeni jijini Dar es Salam, Athman Juma, alisema mke wake alipoteza maisha baada ya mtoto wake kushindwa kupiga simu yenye nywila kuomba msaada wakati mama yake alipozidiwa kwa shinikizo la juu la damu.

Hata hivyo, alisema watu walipofika, mke wake alikuwa ameshafariki kutokana na kukosa msaada wa haraka.

Calvin Joseph, mkazi wa Kibaha alisema simu yake ameweka nywila kwa ajili ya usalama wa vitu vilivyomo ndani.  “Kuna wakati mke wangu huwa anachukua simu na kupekua. Simu isipokuwa na nywila huwa tunagombana sana ndio maana niliamua kuiweka. Sasa hivi akichukua mpaka aniulize nimfungulie. Nywila inasaidia,” alisema.

Mtaalamu wa saikolojia, Frank John alisema wanaopendelea kuweka nywila wanaepuka migogoro ya mahusiano yao.

Habari zaidi soma Gazeti la Mwananchi