Pato la Taifa kufikia Sh104.4 trilioni

Mkurugenzi Mkuu  wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dk Albina Chuwa

Muktasari:

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dk Albina Chuwa amesema iwapo pato hilo lingekokotolewa kwa bei ya mwaka 2007 lingekuwa sawa na Sh47.2 trilioni ikilinganishwa na Sh44.1 trilioni zilizopatikana mwaka jana.

Dar es Salaam. Pato la Taifa kwa bei ya sasa linatarajiwa kukua hadi kufikia Sh104.4 trilioni mwaka huu ikilinganishwa na Sh90.8 trilioni za mwaka jana ikiwa ni ongezeko la Sh13.6 trilioni kutokana na kuwapo viashiria chanya vya ukuaji wa uchumi.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dk Albina Chuwa amesema iwapo pato hilo lingekokotolewa kwa bei ya mwaka 2007 lingekuwa sawa na Sh47.2 trilioni ikilinganishwa na Sh44.1 trilioni zilizopatikana mwaka jana.

Dk Chuwa amesema hali ya uchumi ilizidi kuimarika katika robo ya pili ya mwaka huu (Aprili - Juni) baada ya Pato la Taifa kuongezeka mpaka kufikia Sh11.7 kutoka Sh10.9 trilioni mwaka jana ikiwa ni kutokana na kukua kwa sekta za kilimo na mifugo, shughuli za uchumi na utoaji huduma na sekta ya uchukuzi.

Kwa bei za sasa, pato hilo la robo ya pili ya mwaka huu ni sawa na Sh26.7 trilioni wakati kwa kipindi kama hicho mwaka jana lilikuwa Sh23 trilioni.