Pato la kila Mtanzania sasa Sh2.27 milioni kwa mwaka

Muktasari:

Takwimu hizo za Serikali zinabainisha kuwa ukuaji wa Sh3.4 trilioni wa pato la Taifa ulishamiri kwa asilimia 7.1

Dar es Salaam. Serikali imesema kipato cha kila mwananchi kimeongezeka kutoka Dola 958 za Marekani mwaka 2016 (Sh2.086 milioni) hadi Dola 1,024 sawa na Sh2.276 milioni.

Licha ya kuimarika kwa kipato cha kila mwananchi, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema jana kuwa pato halisi la Taifa limeimarika ndani ya kipindi hicho pia.

Dk Mpango alisema hayo alipokuwa akisoma taarifa ya hali ya uchumi bungeni mjini Dodoma.

Alisema pato hilo liliongezeka kutoka Sh47.1 trilioni mwaka 2016 mpaka Sh50.5 trilioni mwaka jana.

Takwimu hizo za Serikali zinabainisha kuwa ukuaji wa Sh3.4 trilioni wa pato la Taifa ulishamiri kwa asilimia 7.1 ikilinganishwa na asilimia 7.0 za mwaka 2016.

Ukuaji huo, waziri huyo alisema ulichangiwa na utekelezaji wa miradi ya miundombinu, kuongezeka kwa uzalishaji wa baadhi ya madini na kuimarika kwa sekta ya kilimo.

Katika kipindi hicho, Dk Mpango alisema shughuli zilizokua kwa kasi ni uchimbaji madini na mawe kwa asilimia 17.5, usambazaji maji kwa asilimia 16.7, uchukuzi na uhifadhi mizigo kwa asilimia 16.6 na habari na mawasiliano kwa asilimia 14.7.

Shughuli za kilimo cha mazao, ufugaji, uvuvi na misitu zilikua kwa asilimia 3.6 ikilinganishwa na asilimia 2.1 ya mwaka 2016.

Akizungumzia mabadiliko hayo ya kiuchumi kwa mwaka uliopita, mchumi mwandamizi na mtafiti, Profesa Samwel Wangwe alisema kilichosemwa na waziri ni wastani ambao unapaswa kufanyiwa kazi ili kuona uhalisia wake kwenye maisha ya wananchi.

“Kipato cha mwananchi kimeongezeka lakini haijaelezwa kila mmoja amepata kiasi gani. Pamoja na hayo yote, wapo waliopata kidogo na waliopata sana. Kitu muhimu ni kuangalia sekta zilizochangia sana,” alisema Profesa Wangwe.

Alisema kilimo, uvuvi, ufugaji na misitu ni shughuli zinazoajiri watu wengi zaidi hivyo kama kasi yake ya kukua ilikuwa ndogo ni dhahiri kipato cha wahusika hakikuimarika sana.

“Kwenye madini kuna watu wachache. Lakini ni sehemu inayowajumuisha wachimbaji wakubwa na wadogo…kupata hali halisi ni lazima ujue kipato cha wachimbaji wadogo kimeongezeka kwa kiasi gani na wakubwa kimefika wapi,” alisema.

Serikali inatekeleza mpango wa kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025 utakaomruhusu kila mwananchi kuingiza walau Dola 3,000 kwa mwaka.

Akiba

Licha ya kuimarika kwa pato la Taifa na kipato cha kila mwananchi, Dk Mpango alisema akiba ya fedha za kigeni iliongezeka mwaka jana na kupita viwango vilivyopendekezwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Akiba hiyo alisema imeongezeka kutoka Dola 5.9 bilioni za Marekani zinazotosha kuagiza huduma na bidhaa kwa miezi 5.1 kutoka Dola 4.3 bilioni zilizokuwapo mwaka 2016.

Kwa makubaliano ya nchi wanachama wa EAC, waziri alisema kila mwanachama anatakiwa kuwa na akiba inayotosha kuagiza huduma na bidhaa kwa wastani wa miezi 4.5.