Pedeshee Ndama aomba kufutiwa utakatishaji fedha

Muktasari:

Katika kesi hiyo, Ndama anakabiliwa na mashtaka ya kughushi nyaraka za kusafirisha madini na sampuli za madini kwa kusudi la kuonyesha kuwa Kampuni ya Muru iliruhusiwa kusafirisha maboksi manne ya dhahabu kwenda Australia kwa Kampuni ya Trade TJL DTYL Limited wakati akijua si kweli.

Dar es Salaam. Mawakili wa mfanyabiashara Ndama Hussein (44) maarufu Pedeshee Ndama mtoto wa ng’ombe, wameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kulifuta shtaka la sita linalomkabili mteja wao la kutakatisha fedha kwa sababu lina upungufu.

Katika kesi hiyo, Ndama anakabiliwa na mashtaka ya kughushi nyaraka za kusafirisha madini na sampuli za madini kwa kusudi la kuonyesha kuwa Kampuni ya Muru iliruhusiwa kusafirisha maboksi manne ya dhahabu kwenda Australia kwa Kampuni ya Trade TJL DTYL Limited wakati akijua si kweli.

Wakili Jeremiah Mtobesya aliwasilisha hoja hiyo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa. Wakili mwingine wa utetezi ni Wabeya Kundya.

Mtobesya alidai shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili Ndama lina upungufu na kuna taarifa zinakosekana.

Alidai hakuna taarifa zinazoonyesha uhusiano baina ya mshtakiwa na Kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Limited inayodaiwa kulipwa.

Pia, hakuna taarifa zinazomuunganisha mshtakiwa na utoaji fedha kutoka akaunti ya Kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Limited kwenda kwake.

Aliongeza kuwa shtaka hilo halijakidhi matakwa ya kifungu cha 132 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kwa sababu halitoi maelezo ya kutosha kuhusiana na kutakatisha fedha, hivyo lifutiliwe mbali.

Wakili wa Serikali, Christopher Msigwa aliiomba Mahakama iwapo itaona hati ya mashtaka ina upungufu iwape nafasi ya kufanya marekebisho.

Hakimu Nongwa atatoa uamuzi iwapo shtaka hilo lifutwe au la Mei 11.