Penalti yamponza Samatta, baba amuongezea adhabu

Muktasari:

Mbwana Samatta amejikuta akiadhibiwa na baba yake mzazi baada ya kukosa penalti Taifa Stars ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cape Verde jana Jumanne Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Baba mzazi wa mwanasoka wa kimataifa anayekipiga na klabu ya Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta amekuwa akimpa adhabu mwanae huyo pindi inapotokea anakosa penalti.

Mzee huyu anayejulikana kwa jina la Ally Samatta Pazi, amesema tatizo la mwanae kukosa penalti halijaanza leo na awali alikuwa anawalipisha Sh5,000 lakini kwa sasa itakuwa Sh10,000.

Katika mechi ya Stars na Cape Verde iliyochezwa jana Jumanne Oktoba 16, 2018 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Stars kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, Samatta ambaye ndiye nahodha alikosa penalti ambayo Stars iliipata baada ya Msuva kufanyiwa madhambi.

Mzee Samatta anaeleza kwamba adhabu hiyo si kwa Mbwana pekee bali hata kwa kaka yake Mohamed Samatta anayekipiga Mbeya City, akikosa penalti atatakiwa kulipa pesa hiyo.

"Nimewafundisha wakiwa wadogo, najua ubora wao na mapungufu na ndio maana niliwawekea adhabu itakayokuwa inawafanya wawe makini zaidi wanapofikia hatua ya kupiga penalti.

"Nimemshangaa sana Samatta kupiga penalti ovyo dhidi ya Cape Verde anamuona kipa anaruka ruka yeye anaenda kupiga juu, nilijisikia kuchukia kupita kiasi mpaka nikawa naona presha inapanda,"anasema.