Pengo la wanawake kuzibwa baada ya miaka 217

Muktasari:

  • Baraza la Dunia la Uchumi huwalinganisha wanawake na wanaume kwa kuzingatia ushiriki wa kiuchumi, fursa, elimu, uwezeshwaji na afya

Wakati Siku ya Wanawake Duniani ikitarajiwa kuadhimishwa kesho, ripoti ya hivi karibuni iliyotolewa na Baraza la Dunia la Uchumi (WEF), imebaini kuwa kuna tofauti kubwa kati ya wanawake na wanaume katika maeneo mengi na itachukua miaka 217 kuliondoa pengo hilo.

Kila mwaka, baraza hilo hufanya utafiti kwa kuangalia uwiano wa kiuchumi kati ya wanawake na wanaume katika nchi 144 duniani na kuwalinganisha kwa kuzingatia nguzo nne ambazo ni ushiriki wa kiuchumi, fursa, elimu, uwezeshwaji na afya.

Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa Machi 8 kila mwaka na kauli mbiu ya mwaka huu ni, ‘Wakati ni huu: wanaharakati wa mjini na vijijini kubadili maisha ya wanawake.’

Baraza hilo, huchukua taarifa kutoka katika mashirika makubwa kama la Kazi Duniani, (ILO), Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) na Shirika la Afya Duniani.

Ripoti ya baraza hilo inaonyesha kuwapo kwa pengo kubwa kati ya wanawake na wanaume, katika maeneo ya mishahara, ushiriki katika kazi na katika uongozi kuna pengo kubwa linalokua kwa kasi zaidi.

Ripoti hiyo imetolewa Novemba 20 mwaka jana na kubaini kuwa pengo la kiuchumi kati ya wanawake na wanaume halitazibika kwa miaka 217 ijayo.

Ripoti hiyo imebaini kuwa wanaume wapo juu katika maeneo hayo ya ajira, uchumi, afya, mishahara, nafasi za uongozi na biashara kuliko wanawake.

Wanaharakati wa masuala ya jinsia wamezungumzia pengo hilo kubwa kati ya wanawake na wanaume na wakataja chanzo na suluhisho.

Dk Joyce Bazira, Mratibu wa Mradi wa Wanawake katika Habari Tanzania, (WIN) amesema juhudi za ziada zinatakiwa kwani tatizo la utofauti kati ya wanawake na wanaume ni kubwa.

“Siwezi kusema itachukua miaka mingapi, lakini ni kitu ambacho kitafanyika kidogo kidogo.” alisema.

Dk Joyce ambaye pia ni mwanahabari mkongwe, alisema ni vizuri kuangalia chanzo cha tatizo kwa kuwa suala la jinsia limeanzia katika mifumo ya mababu zetu.

“Lazima tujiulize ni kitu gani kimefanya tofauti iwe kubwa? Tatizo ni nini katika kila eneo? Itachukua muda kwa kweli, siyo kitu cha siku moja,” alisema Dk Bazira.

Alifafanua kwamba wanawake walio nyuma lazima waweke juhudi za ziada kwani anayeumizwa na kiatu, ndiye anayejua maumivu yake.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi alisema kwamba unahitajika utashi wa kisiasa ili kuhakikisha mwanamke anakwenda sambamba na wanaume katika maeneo hayo.

“Inaonekana kama itachukua miaka mingi kwa sababu hakuna mwamko wala dhamira ya dhati katika suala hili, hakuna ushirikishwaji wa mwanamke katika maeneo mengi,” alisema Liundi.

Alifafanua kuwa licha ya kuwapo rasilimali za kutosha, lakini inaonekana itachukua miaka mingi kwa sababu wanawake wanaachwa nyuma.

Alitoa mfano wa takwimu za mwaka 2012, akisema zinaonyesha kwamba idadi ya wanawake pekee nchini ni asilimia 51.3 lakini bado hawashiriki masuala ya maendeleo.

Liundi alisema kwamba kukiwa na kundi kubwa lakini halishiriki lazima kutakuwa na kasoro.

“Lakini hii miaka inayotajwa ni kwa sababu hakuna dhamira ya dhati kuanzia katika ngazi ya familia. Mifumo yote isimkandamize mwanamke.

Kimsingi, siku hiyo (ya wanawake duniani) ilianza kwanza kwa kuitwa siku ya wafanyakazi wanawake ya kimataifa na ilikuwa inaadhimishwa kila Machi 8.

Lengo la maadhimisho lilikuwa ni kumuonyesha upendo na heshima mwanamke kutokana na mafanikio yake katika nyanja mbalimbali kama vile siasa, kijamii na kiuchumi.

Ni siku ambayo wanawake hutambuliwa kutokana na mafanikio yao bila kujali mgawanyiko wa taifa, kabila, lugha, itikadi, kitamaduni, kiuchumi au kisiasa.