Polepole: CCM kuisimamia Serikali ili kuimarisha usafiri Ziwa Victoria

Muktasari:

Polepole amesema CCM itahakikisha inaisimamia Serikali ili miundombinu ya usafiri wa Ziwa Victoria unaimarika

Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Humprey Polepole amesema kama chama kitaendelea kuisimamia Serikali ili kuhakikisha miundombinu au usafirishaji katika Ziwa Victoria unaimarika na kuweka sheria za kusimamia uendeshwaji wa vyombo vya majini

Hayo amesema leo Septemba 23,2018 wakati akitoa salamu wa mazishi ya baadhi ya watu waliopoteza maisha katika ajali ya Kivuko cha Mv Nyerere, Ukara wilayani Ukerewe Mkoa wa Mwanza.

Polepole amesema hatua hiyo imefikiwa kutokana na kutokuwa tayari kuona wanapoteza nguvu kazi ya Watanzania kila wakati kutokana na vitu vinavyoweza kuzuilika.

"Sote tumejawa na simanzi lakini tunamuomba Mungu aweze kuwapa nguvu wafiwa katika kipindi hiki kigumu," amesema Polepole.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais-Zanzibar, Muhammed Aboud Mohammed akisoma salamu za pole na rambirambi kutoka kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohammed Shein, alitoa pole kwa Watanzania wote walioguswa na msiba huo sambamba na kuwaombea waliojeruhiwa ili waweze kupona haraka.

 

"Pia, tunawashukuru na kuwapongeza watu wote walioshiriki katika shughuli hili wakiwamo waokoaji, askari pia wahudumu wa afya wanaoendelea kutoa huduma kwa majeruhi," amesema.

 

Pia, aliwataka wananchi kuwa na subira katika kipindi hiki kwa sababu kila jambo linatoka kwake.