Sunday, October 7, 2018

Polepole: Wabunge wanaotaka kuhamia CCM mwisho Desemba 2018

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole. 

Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema wabunge wa upinzani wanaotaka kujiunga na chama hicho tawala mwisho wa kufanya hivyo ni Desemba, 2018.

Polepole amesema mwaka 2018 ndio mwisho wa chaguzi ndogo za ubunge, wale watakaoshindwa kuhamia CCM wabaki walipo.

Polepole ametoa maelezo hayo leo Jumapili Oktoba 7, 2018 katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter huku baadhi ya watu wakikosoa kauli yake hiyo, wakibainisha kuwa CCM kimepoteza umaarufu.

“Tumezingatia na tunaweka jitihada zetu zote katika kushughulika na utatuzi wa shida za watu wetu wa Tanzania. Mwaka 2018 ndiyo mwisho kwetu kufanya chaguzi ndogo za ubunge kwa wale wanaohama vyama vyao na kujiunga na CCM. Watakaoikosa raundi hii mbaki hukohuko tutakutana 2020.”

Wakati Polepole akieleza hayo, hadi sasa wabunge saba wa upinzani wamevihama vyama vyao na kujiunga na CCM, akiwemo mbunge wa Simanjiro (Chadema), James Ole Millya aliyejiunga CCM leo.

Wabunge hao ni Maulid Mtulia (Kinondoni), Dk Godwin Mollel (Siha), Julius Kalanga (Monduli), Mwita Waitara (Ukonga). Wanne hao walipojiunga CCM walipitishwa kuwania ubunge na kuibuka na ushindi.

Wengine ni Zuberi Kuchauka (Liwale) ambaye pia amepitishwa na CCM kuwania ubunge katika jimbo hilo kwenye uchaguzi utakaofanyika Oktoba 13, 2018. Mwingine ni Marwa Chacha aliyekuwa mbunge wa Serengeti kwa tiketi ya Chadema.

Wamkosoa Polepole

Henry Kileo ni baadhi ya waliojibu ujumbe huo wa Polepole na kusema; “Hiyo project yenu ya ununuzi wa wanasiasa imewashikisha adabu kwa kuwaonyesha msivyochaguliwa zaidi ni kupora. Katibu Mkuu wenu kaweka hadharani mambo yote, hamna uhalali wa kisiasa kuongoza. Sijui unazungumziaje kauli hiyo ya Boss wako.”

Joseph Mauki amesema, “nini mantiki ya Tweet kama hii kwa kiongozi kama wewe? Wahame haraka haraka ambao wameshapokea gawio au wafanye mpango wa kuchukua fomu kwako kwa watakaohitaji?”

Marwa Aruni amesema, “nyinyi hamshughulikii shida za wananchi bali biashara za siasa. Tangu tupate uhuru hatujawahi kufanya chaguzi za kijinga kama hizi ambazo zimetafuna robo ya pato letu. Tumechoka ndio maana hatuendi kupiga kura. Naungana na katibu mkuu wenu kuwa hamna uhalali kutawala.”

-->