Polepole apinga sherehe ya Makonda, polisi

Muktasari:

  • Juzi, mara baada ya Mwita Waitara kutangazwa mshindi wa ubunge wa Ukonga kupitia CCM akimshinda mshindani wake wa karibu kutoka Chadema, Asia Msinga, Makonda na askari waliovalia sare za jeshi hilo walipongezana kwa kugongesha soda na kumnyanyua juu mkuu huyo wa mkoa.

Dar es Salaam. Hatua ya mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kupongezana hadharani kwa kulinda amani kabla na baada ya uchaguzi wa ubunge Jimbo la Ukonga, imemuibua katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole kupinga.

Pamoja na Polepole pia wadau wengine wamepinga kitendo hicho.

Juzi, mara baada ya Mwita Waitara kutangazwa mshindi wa ubunge wa Ukonga kupitia CCM akimshinda mshindani wake wa karibu kutoka Chadema, Asia Msinga, Makonda na askari waliovalia sare za jeshi hilo walipongezana kwa kugongesha soda na kumnyanyua juu mkuu huyo wa mkoa.

Katika sherehe hiyo iliyofanyika eneo la kituo kikuu cha polisi cha kanda hiyo, Makonda aliwapongeza kwa kazi kubwa ya kuimarisha ulinzi na usalama kipindi cha kampeni na baada ya uchaguzi uliofanyika Septemba 16.

Kila alipokuwa akitoa pongezi hizo, askari walikuwa wakisema maneno ya kuhamasishana kwa kusema “abebwe abebwee” na wakambeba juujuu wakicheza na kurukaruka.

Kisha Makonda alisema, “tutapiga chiazi ya kumaliza uchaguzi kwa usalama na amani.”

Polepole ampinga

Jana katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole akizungumzia ushindi wa chama hicho kwa majimbo ya Ukonga na Monduli pamoja kata 23 nchini, mbele ya wanahabari katika ofisi ndogo za Lumumba, Dar es Salaam, Polepole alisema Makonda hakupaswa kufanya sherehe na askari.

Alisema sherehe hiyo ingekuja baadaye kwa sababu askari waliopongezwa kuna wakati walishindwa kuchukua hatua pale sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) zilipokiukwa.

Alisema kuna wakati alimfuatilia mgombea wa Chadema, Msangi, akitoa vitisho kwa wasimamizi wa uchaguzi ambapo alitweza utu na mamlaka ya wasimamizi wa uchaguzi na askari waliokuwepo hawakuchukua hatua.

“Makonda hakupaswa kufanya sherehe nao (askari) kwa sababu kuna mahali sheria ya tume zilikuwa zinakiukwa na wao wapo wametulia,” alisema Polepole.

“Si wanasema askari wanasaidia CCM, sasa katika mazingira ambayo msimamizi wa kituo cha kupigia kura anakwidwa na watu waliofanya hivyo hawajakamatwa kupelekwa kwenye vyombo vya sheria ili haki ikapatikane.”

“Unazungumza na mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa namba ya mgombea unamlazimisha msimamizi wa kituo afanye vinginevyo tofauti na utaratibu kwa simu ya mgombea, nilifikiri pale nilitaka tulinde mamlaka sherehe ingekuja baadaye kidogo.”

TLS wasema ni aibu

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume alisema kitendo kilichofanywa na mkuu huyo wa mkoa pamoja na askari hao ni aibu na kinyume cha sheria.

“Kisheria kazi yao ni kulinda usalama wa raia na mali zao na si vinginevyo. Kitendo walichokifanya hakionyeshi weledi wa kazi yao,” alisema Fatma.

“Kibaya zaidi wakati wanafanya hayo walikuwa wamevaa sare za kazi na kofia juu, halafu wanapongezana na kiongozi wa nafasi ya kuteuliwa na Rais ambaye ana mlengo wa kisiasa, na wao bila shaka wanaonyesha kuwa na mlengo huo.”

Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mohammed Bakari alisema kitendo walichokifanya askari hao hakikuwa sahihi kwa sababu hakuna sheria inayowaruhusu kufanya hivyo.

“Kitendo hicho kinathibitisha wanaunga mkono mlengo wa CCM kwa sababu waliyekuwa wakishangilia naye ameteuliwa na wa mlengo huo,” alisema Profesa Mohamed.

Alisema, “unaposhangilia kumalizika salama uchaguzi hadharani na unabebwa juujuu na walinda usalama wa nchi inaonyesha mnafurahia pamoja na ushindi wa chama kilichowapa kazi na kuwateua.”