Monday, June 19, 2017

Polepole awajia juu viongozi miungu watu CCM

Katibu Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey

Katibu Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole akizungumza wakati wa ufunguzi wa darasa la itikadi na uenezi kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu wa Mkoa wa Dar es Salaam lililofanyika Pugu wilayani Ilala, jana. Picha na Omar Fungo 

By Raymond Kaminyoge, Mwananchi rkaminyoge@mwananchi.co.tz

Ikiwa bado ina majonzi ya kupoteza majimbo kadhaa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, CCM imewaagiza wanachama wake kuwatosa viongozi miungu watu waliosababisha majimbo na kata kuchukuliwa na vyama vya upinzani.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema jana baadhi ya majimbo na kata zilichukuliwa na vyama vya upinzani kwa sababu ya viongozi waliojitenga na wanachama wao.

Alisema chama hicho kimeanza kuondoa viongozi wa ovyo na kitaendelea kufanya hivyo kwa awamu.

Tangu kumalizika kwa uchaguzi huo, chama hicho kimekuwa kikiwavua madaraka baadhi ya viongozi wake wa ngazi mbalimbali na kuwafuta uanachama makada ambao walikwenda kinyume na maadili ya chama hicho au kusababisha kukosa majimbo katika uchaguzi wa 2015.

Miongoni mwa waliovuliwa uanachama ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sophia Simba ambaye pia alikuwa Mbunge wa Viti Maalumu hivyo kupoteza nyadhifa zake zote.

Februari mwaka huu, CCM Mkoa wa Arusha iliwavua uanachama makada wake 1,520 kwa tuhuma mbalimbali ikiwamo kukisaliti chama hicho.

Jana, akifungua darasa la itikadi na uenezi kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu wa Mkoa wa Dar es Salaam lililofanyika Pugu wilayani Ilala, Polepole alisema CCM ni mali ya wanachama.

Akitoa mfano, Polepole alisema Jimbo la Ukonga na kata zake nyingi zilichukuliwa na vyama vya upinzani kwa sababu baadhi ya viongozi waliona chama ni mali yao binafsi.

“Wanachama wa CCM wakakasirika wakavipigia kura vyama vya upinzani, tusirudie makosa tuanze kujisafisha wenyewe kwa kuwang’oa viongozi mabwanyenye,” alisema.

Polepole alisema ushahidi wa hilo ni kuwa jimbo hilo lina wana CCM wengi kuliko wanachama wa vyama vingine lakini cha kushangaza lilichukuliwa na Chadema huku kata saba zikichukuliwa na vyama vya upinzani na CCM kuambulia sita.

Polepole aliwaonya wanaotafuna mali za chama akisema siku zao zinahesabika, “Kuna viongozi wa chama minyoo, wanatafuna mali za chama, wako kwenye chama kwa masilahi binafsi tutapambana nao.”

Awali, Makamu Mwenyekiti wa vyuo vikuu Mkoa wa Dar es Salaam, Asha Feruzi alisema lengo la mkutano huo ni kuwapa wanachama elimu ya itikadi na uenezi.

Alisema washiriki wa mkutano huo ni wanavyuo mbalimbali wa Dar es Salaam na wanachama wanaoishi katika Wilaya ya Ilala.

-->