Polepole awakaribisha wanaokimbia upinzani

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Humphrey Polepole

Muktasari:

  • Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema kwamba wapinzani wameonyesha utovu wa nidhamu hivyo awahakikishia anawapokea waliohama.

Bagamoyo. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Humphrey Polepole amesema anayo orodha ndefu ya viongozi wa upinzani wanaotaka kuhamia CCM.

Polepole amesema hayo leo huku akibainisha kuwa orodha hiyo inahusisha wenyeviti, madiwani na wabunge lakini siku nyingi tu alikuwa amewakatalia kuwapokea.

Hata hivyo Polepole amesema kwamba kutokana na kutuhumiwa kuwanunua sasa anafanya kweli, atawachukua mmoja mmoja.

Polepole amesema amemua kuchukua uamuzi huo baada ya Chadema kuonyesha utovu wa nidhamu kwa kudai kuwa madiwani wanaokihama chama hicho wamehongwa na CCM.

“Sasa tutaanza kumchomoa mmoja baada ya mwingine na kwa kutekeleza hilo wiki hii watampokea kiongozi mkubwa wa chama hicho,’’anasema Polepole.

Amebainisha kuwa kama chama kinakuwa na viongozi wanaoweza kuhongwa na wakahongeka basi  chama hicho kitakuwa ni cha hovyo
"Madiwani wamesema wanamuunga mkono John Magufuli, wametoka wenyewe wameanza kusema CCM imewanunua, sasa kwa vile wameanza utovu wa nidhamu nitaanza kumtoa mmoja baada ya mwingine,’’anasema.

Polepople anaongeza kwamba: “Nilikua nakataa kuwapokea ila nina orodha kubwa wapo wenyeviti, wabunge kibao kama vile watu wanaojisaliji kodi ya majengo TRA," amesema.
"Unajua wanasema wanaisoma namba, nawahakikishia baada ya miaka mitano kwa spidi hii iliyoanza nayo CCM namba inayoonekana wakati huu itakuwa haisomeki kabisa, nitafanya shoo ndogo tu kuwachomoa viongozi hao sipendi kwenda kuwachukua wengi sababu nitaonekana kama nawahujumu vile na pia ili upinzani usikose watu angalau wa kuzungumza nao,"amesema