Taasisi hizi zimekithiri kwa rushwa

Muktasari:

Amesema Takukuru katika kipindi hicho imepokea jumla ya taarifa 219 za rushwa kwa njia mbali mbali.


Dar es Salaam. Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)Ilala,  Zainabu  Bakari amesema taasisi zinazolalamikiwa zaidi kwa rushwa ni Polisi, Idara  ya Mahakama, Wizara ya Ardhi,Idara ya Afya , Tamisemi, Kampuni za Bima na sekta binafsi.

Bakari ameeleza hayo leo Aprili 19 wakati akizungumzia utendaji wao wa kazi katika kipindi cha Julai 2017 na Machi 2018.

Amesema Takukuru katika kipindi hicho imepokea jumla ya taarifa 219 za rushwa kwa njia mbalimbali zikiwamo simu 113 pamoja na watu kufika ofisini kwao, barua na barua pepe.

 Amesema uchunguzi wa taarifa hizo unaendelea na upo katika hatua mbali mbali.

Amesema majalada yaliyofunguliwa ni 24, majalada yaliyokamilika 14, majalada yaliyopelekwa kwa mkurugenzi wa mashtaka kuombewa kibali saba na yaliyopata kibali  ni matatu.

Amesema mpaka sasa wamefikisha kesi nane mahakamani za kuomba na kupokea rushwa  na kwamba sita zilitolewa maamuzi na wakashinda.