Polisi, Mahakama zaongoza kwa rushwa

Muktasari:

CAG wa zamani, Ludovick Utouh ametaka mamlaka za mapambano ya rushwa kuheshimu utu na haki za binadamu.

Utafiti uliofanywa na taasisi ya Twaweza unaonyesha kiwango cha rushwa kimepungua kwa asilimia 85 ikilinganishwa na miaka mitano iliyopita, huku Polisi na Mahakama zikiongoza kwa kupokea rushwa.

Mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze amesema hayo leo Jumatano Novemba 22,2017 akiwasilisha matokeo ya utafiti huo uliofanyika kati ya Julai na Agosti kwa upande wa Tanzania Bara ambao ulipewa jina la "Hawashikiki"?

Eyakuze amesema wahojiwa walikuwa 1,705 ambao wamesema rushwa imepungua katika sekta zote mwaka 2017 ikilinganishwa na mwaka 2014.

"Pamoja na mtazamo wa wananchi kwamba rushwa imepungua, sekta za Polisi na Mahakama bado zinaongoza kwa rushwa. Asilimia 39 na asilimia 36 ya wananchi wanasema waliombwa rushwa mara ya mwisho walipokutana na taasisi hizo mbili," amesema Eyakuze.

Ametaja kiwango cha rushwa kilivyokuwa mwaka 2014 na mwaka huu kuwa Polisi asilimia 39 kutoka asilimia 60, ardhi asilimia 18 kutoka asilimia 32, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) asilimia tano kutoka asilimia 25 na afya asilimia 11 kutoka asilimia 19.

"Utoaji wa rushwa wakati wa kampeni asilimia 93, utoaji wa fedha au vitu kwa ajili ya kupata huduma asilimia 78, kuwalipa wafanyakazi hewa asilimia 65. Asilimia 51 wamesema posho za vikao ni rushwa," amesema Eyakuze.

Mkurugenzi huyo amesema wahojiwa wamesema itumike njia sahihi katika mapambano dhidi ya rushwa.

Amesema asilimia 65 wamesema kila mtu anapaswa kupewa nafasi ya kujitetea, huku asilimia 35 wanasema haki za msingi za mtuhumiwa zinaweza kuwekwa kando.

Mwakilishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Sabina Seja amesema, "Siwezi kusema moja kwa moja rushwa imepungua au imeongezeka ila niseme tu rushwa ipo."

Amesema, "Bado vitendo vya rushwa vipo na kila mmoja anapaswa kutambua madhara yake. Tunawaomba waendelee kutupatia ushirikiano."

Mkurugenzi Mtendaji wa JamiiForum, Maxence Melo amesema mapambano dhidi ya rushwa yanapaswa kushirikisha wadau wote katika jamii na Serikali iepuke kusema jukumu hilo ni lao peke yao.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wa zamani, Ludovick Utouh amesema ni kweli vitendo vya rushwa vimepungua.

Hata hivyo, amezitaka mamlaka zinazoshughulikia mapambano ya rushwa kuheshimu utu na haki za binadamu.

Amesema kutuhumiwa kwa rushwa ni jambo moja na kubainika kula rushwa ni jambo jingine.