Polisi ‘wammulika’ Mbowe

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe

Muktasari:

Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro  amesema jana kuwa Mbowe kupitia kwa baadhi ya viongozi aliwajulisha angeripoti Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, Jumatano Februari 15, akakubaliana na taarifa hiyo lakini hajaripoti mpaka sasa.

Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa endapo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe hataripoti polisi kesho, atatafutwa kwa namna ambayo jeshi hilo litaona inafaa.

Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro  amesema jana kuwa Mbowe kupitia kwa baadhi ya viongozi aliwajulisha angeripoti Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, Jumatano Februari 15, akakubaliana na taarifa hiyo lakini hajaripoti mpaka sasa.

Mbowe, ni miongoni mwa watu mashuhuri na wafanyabiashara waliotajwa hivi karibuni katika orodha ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ya watu 65 wanaodaiwa kujihusisha na dawa za kulevya.

 “Mheshimiwa Mbowe tunamheshimu sana kama kiongozi wa chama kikubwa cha siasa na hata akiwa bungeni ameonekana akipinga kwa nguvu suala la dawa za kulevya na anasikitika kuona vijana wa Kitanzania wanateketea. Asitafute namna nyingine, tunamhitaji kwa ajili ya kumhoji kutokana na hizi tuhuma za dawa za kulevya,” amesema Sirro.