Polisi watawanya wafuasi wa Nasa

Muktasari:

Hadi saa 3:00 asubuhi waandamanaji walikuwa wamejikusanya eneo la Kondele wakijiandaa kuelekea ofisi za IEBC zilizoko Milimani mjini Kisumu.

Nairobi, Kenya. Mapambano yamezuka kati ya polisi na wafuasi wa muungano wa upinzani (Nasa) walioandamana kuendelea kushinikiza maofisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) waondoke ikiwa ni siku moja baada ya kukaidi amri ya serikali.

Serikali jana ilipiga marufuku maandamano ya wapinzani katika miji ya Nairobi, Kisumu na Mombasa lakini leo waandamanaji hao wamekaidi na wakajimwaga mitaani ambako baadhi ya maeneo walichoma matairi barabarani.

Mjini Mombasa, polisi wa kuzuia ghasia walijaa katika mitaa ya mji huo ulioko pwani ili kusimamia maelekezo ya serikali ya kuzuia maandamano hayo.

Polisi hao waliwatawanya wafuasi wa Nasa waliokusanyika eneo la Uhuru Gardens katika Mtaa wa Moi na baadaye Barabara ya Nkrumah.

Naibu Gavana William Kingi, Seneta Mohammed Faki na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir walikuwa wakiongoza maandamano hayo polisi walipofika na kuwarushia mabomu ya kutoa machozi. Waandamanaji hao walikimbia hovyo kwa ajili ya usalama wao huku polisi wakiwafukuzia.

Haikuweza kufahamika mara moja ikiwa kuna watu waliokamatwa au waliojeruhiwa katika vurumai hiyo.

Kulikuwa na dalili za kuwepo maandamano katika miji ya Nairobi na Kisumu ambako serikali imeyapiga marufuku katika miji yenye shughuli nyingi za kibiashara.

Mjini Kisumu, wafuasi wa ODM ambao ni washirika wa Nasa walisema wanajipanga kufanya maandamano katika maeneo yote yenye shughuli za kibiashara. Seneta wa Kisumu Fred Outa ameliambia gazeti la Nation kwamba wangefanya maandamano kila mahali katika mji huo.

Kwa mujibu wa Outa, Kaimu Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang’I aliyepiga marufuku maandamano hana mamlaka juu ya Katiba “inayowapa haki ya kugoma”.