Polisi aeleza alivyoagizwa kumkamata Halima Mdee

Muktasari:

Adai kuwa kabla ya kumkamata Mdee alikuwa hajawahi kumuona ana kwa ana

Dar es Salaam. Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Urafiki, mrakibu wa polisi (SP) Batseba Kasanga ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa aliagizwa kwenda kumkamata Halima Mdee nyumbani kwa wazazi wake kwa tuhuma za kutoa lugha chafu dhidi ya Rais John Magufuli.

Shahidi huyo alidai kuwa Julai 4, 2017 alipokea agizo hilo kutoka kwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kinondoni, Mark Njela.

Shahidi huyo wa tatu wa upande wa mashtaka alisema hayo jana alipokuwa akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Patrick Mwita kutoa ushahidi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba.

Inadaiwa Julai 3, 2017 katika makao makuu Chadema, Mdee alitamka maneno ya kumkashfu Rais Magufuli kwamba: “Anaongea hovyo hovyo, anatakiwa afungwe brek.”

Akisimulia alipokwenda kumkamata mtuhumiwa huyo nyumbani kwa wazazi wake Ubungo Kibangu, shahidi alidai kuwa walitumia gari la doria akisaidiana na askari wawili; walipofika walipokewa na kaka wa Halima ambaye aliwaelekeza kwa mama yao.

Alisema walipoonana na mama mzazi wa mbunge huyo, aliwaeleza wamsubiri kidogo Halima anajiandaa kwa kuwa alikuwa amepumzika.

Kasanga alidai baada ya hapo Halima alitoka na wakamueleza kuwa wamekwenda kumkamata na kumpeleka Oysterbay Polisi.

Alidai kuwa walipofika Oysterbay Polisi, Njela hakuwapo hivyo alimpigia simu na akamuelekeza amkabidhi Mdee kwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Ilala (RCO), Davis Msangi.

Shahidi huyo amedai kuwa baada ya kumkabidhi kwa Msangi aliondoka na kurudi kituoni kwake kuendelea na majukumu yake.

Hata hivyo, alieleza kuwa kabla ya kumkamata alikuwa hajawahi kumuona Mdee ana kwa ana na alikuwa akimsikia katika vyombo vya habari ikiwamo televisheni na magazeti.

Katika kesi hiyo, Mdee anatetewa na mawakili Peter Kibatala na Hekima Mwasipu ambaye alimuuliza shahidi huyo kuwa tangu tarehe aliyomkamata hadi sasa alishawahi kuyasikia maneno yaliyotamkwa na Halima Mdee.

Kasanga alijibu: “Kwa kweli sikuwahi kuyafuatilia.”

Kesi iliahirishwa hadi Septemba 11, 2018; mashahidi wa upande wa mashtaka watakapoendelea kutoa ushahidi.