Polisi agonga mtu kwa baiskeli, afariki dunia

Muktasari:

Tukio hilo la kusikitisha limetokea Mkoa wa Manyara na kuwashangaza wengi walioshuhudia

 


Babati. Askari polisi wa Kituo cha Babati mkoani Manyara, Boniface Masunga (32) amefariki dunia baada ya baiskeli aliyokuwa akiendesha wakati akielekea kazini kumgonga mtembea kwa miguu.

Baada ya kumgonga mtu huyo, askari huo aliangukia  kichwa na kufariki dunia papo hapo.

Akizungumza leo Jumamosi Machi 24, 2018, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Manyara, Agostino Senga amesema tukio hilo limetokea jana katika barabara kuu ya Babati-Singida.

Amemtaja aliyegongwa kuwa ni Awadhi Ashraf (20) mkazi wa mjini Babati na kwamba, chanzo cha ajali hiyo ni Ashraf ambaye ni fundi ujenzi kuingia barabarani bila kuchukua tahadhari.

"Huyo fundi alikuwa anaingia kwenye barabara kuu ya lami bila kuchukua tahadhari, hivyo akagongwa na baiskeli aliyokuwa anaendesha polisi huyo," amesema Kamanda Senga.

"Tukio hilo lililotokea ghafla sana kwani alivyomgonga aliangukia kichwa na kuanza kutokwa damu masikioni.”

Hata hivyo, baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo walishangazwa na ajali hiyo kwani hawajawahi kuona mtu akagongwa na baiskeli na mwendeshaji kufa.

Mkazi wa eneo la Sawe mjini Babati, Mariki John amesema tukio hilo ni la kushangaza kwani askari huyo japo alikuwa mdogo kiumri, lakini baiskeli imesababisha kifo chake.