Polisi waanza uchunguzi kutekwa mwanafunzi UDSM -VIDEO

Muktasari:

  • Baada ya kuhojiwa Nondo amesema kuwa alitekwa na watu wasiojulikana ambao walimtekeleza  Wilaya ni Mufindi

Mafinga. Jeshi la Polisi mkoani Iringa limefungua jalada la uchunguzi kwa lengo la kubaini ukweli juu ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Abdul Nondo anayedaiwa kutekwa na watu wasiojullikana na kutelekezwa wilayani Mufindi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 8 ofisini kwake mjini hapa, kamanda wa polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire amesema Nondo aliripoti kituo cha polisi cha Mafinga wilayani Mufindi jana  saa moja jioni.

“Baada ya kumhoji Nondo alisema kuwa alitekwa na watu wasiojulikana ambao walimtekeleza  Wilaya ni Mufindi,” amesema kamanda huyo.

Nondo (24) ambaye ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP) na mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alitoweka juzi katika mazingira ya kutatanisha. Mara ya mwisho alionekana jijini Dar es Salaam.

“Tunaendelea kufanya uchunguzi kama ametoa taarifa za uongo kwa nia ovu kwa lengo la kutaka kuhamasisha wanafunzi wenzake ili kuleta uvunjifu wa amani nchini tutamshughulikia kama wahalifu wengine," amesema Bwire.

Amesema kama kweli mwanafunzi huyo atakuwa ametekwa jeshi hilo litawasaka watuhumiwa na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Kamanda Bwire amewaomba wananchi wenye taarifa mbalimbali kuhusiana na tukio hilo watoe ushirikiano  ili kukamilisha uchunguzi huo mapema.