Polisi wafanya upekuzi nyumbani kwa Zitto

Muktasari:

Polisi wamefanya upekuzi nyumbani kwa mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe  na kumrudisha katika kituo cha Oysterbay kutoka Kituo Kikuu

 


Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Mkoa wa kipolisi Kinondoni limefanya upekuzi nyumbani kwa Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe.

Jebra Kambole, wakili wa mbunge huyo wa Kigoma Mjini amelieleza Mwananchi leo Alhamisi Novemba Mosi, 2018  kuwa upekuzi huo umefanyika Masaki jijini hapa, nyumbani kwa mbunge huyo.

Jana saa tatu asubuhi Zitto alikamatwa na polisi akiwa nyumbani kwake na kupeleka katika Kituo cha polisi Oysterbay ambako alihojiwa kwa saa tatu na kuhamishiwa kituo kikuu cha polisi.

Kambole amesema baada ya mteja wake kupelekwa kituo kikuu cha polisi, hakulala hapo alihamishiwa kituo kingine kilichopo Mburahati ambako aliondolewa leo asubuhi na kurudishwa kituo cha polisi Oysterbay.

“Leo asubuhi mteja wangu aliongozana na polisi hadi nyumbani kwake Masaki kwa ajili ya kufanya upekuzi kisha akarudishwa kwenye kituo cha Oysterbay,” amesema.

“Bado tunashughulikia suala la dhamana ya mteja wangu. Ila kwa dalili ninavyoziona sijui kama polisi watampa dhamana siku ya leo.”

Wakati huohuo, Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Seleman Bungala maarufu ‘bwege’ amempa pole Zitto na kubainisha kuwa wapo naye pamoja.

Soma zaidi: