Msako waliomuua tajiri wa mabasi waendelea

Muktasari:

  • Jeshi hilo pia linaendelea kuwahoji watu wanne wanaoshikiliwa kuhusiana na tukio hilo.

Jeshi la Polisi linaendelea na msako dhidi ya watu wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya mfanyabiashara na mmiliki wa kampuni ya mabasi ya Super Sami, Josia Mzuri maarufu kwa jina la Samson ambaye mwili wake ulikutwa kwenye viroba ndani ya Mto Ndabaka mpakani mwa wilaya za Bunda na Busega.

Akizungumza kwa njia ya simu leo Machi 23, Kamanda wa Polisi mkao wa Mara, Jaffari Mohamed alisema pamoja na msako dhidi ya watuhumiwa wengine, jeshi hilo pia linaendelea kuwahoji watu wanne wanaoshikiliwa kuhusiana na tukio hilo.

Ametoa wito kwa wenye taarifa zitakazosaidia kuwanasa wahusika au kufanikisha ushahidi dhidi ya watuhumiwa wanaoshikiliwa kujitokeza kuziwasilisha polisi.

“Suala hili linahitaji uchunguzi wa kina si tu kubaini na kuwanasa wahusika, bali pia kupata ushahidi wa kina unaotosheleza kuwatia hatiani, tunaomba raia wema washirikiane na polisi kukamilisha jukumu hilo,” amesema Kamanda Mohamed.

Tajiri huyo alizikwa nyumbani kwake Majengo ya Chini wilayani Magu mkoani Mwanza huku baadhi ya wafanyabiashara wenzake wakielezea kuingiwa hofu ya usalama na maisha yao.

Hofu ya wafanyabiashara na wamiliki wa mabasi ya abiria mkoani Mwanza ilitolewa na Joseph Kasheku ‘Msukuma’ alipozungumza kwa niaba ya wenzake siku ya mazishi Machi 16 na kuomba vyombo vya dola kuchunguza suala hilo ili kubaini wahusika na sababu za kufanya hivyo.

“Mauaji haya yameibua hofu na wasiwasi mwingi miongoni mwetu wafanyabiashara ya usafirishaji wa abiria mkoani Mwanza kwa sababu hatujui kwanini mwenzetu katekwa na kuuawa wala hatuelewi nani atafuata,” alisema Msukuma.

Mfanyabiashara huyo alitoweka tangu Februari 27, siku moja baada ya kushiriki kikao cha Kamati ndogo ya Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), mkoani Mwanza kilichofanyika jijini Mwanza Februari 26.

Gari la mmiliki huyo wa mabasi, Machi 9 lilikutwa likiwa limeteketezwa kwa moto ndani ya eneo la eneo la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara, siku tano kabla ya mwili wake kukutwa ndani ya maji katika Mto Ndabaka ukiwa umefungwa kwenye viroba.