Monday, January 8, 2018

Polisi wakumbushia matukio matatu mkoani Mbeya

kamanda wa polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed

kamanda wa polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga 

By Godfrey Kahango, Mwananchi gkahango@mwananchi.co.tz

Polisi Mkoa wa Mbeya imesema mwaka 2017 ulikumbwa na matukio mengi, lakini matatu ndio yaliyoutikisa na kuvuta hisia za wananchi wengi kutokana na namna yalivyozua taharuki katika jamii.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari ofisini kwake jijini hapa, kamanda wa polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga alisema matukio hayo ni pamoja na waombolezaji kuzika jeneza likiwa tupu bila mwili wa marehemu, mzazi kufukua kaburi la mtoto na kutoa mwili na kwenda kuuhifadhi nyumbani kwa imani atafufuka pamoja na kuteketea kwa moto soko la Sido lililopo Mwanjelwa.

Kamanda Mpinga alisema tukio la kwanza ni lile la waombolezaji kuzika jeneza tupu na mwili wa marehemu, Harun Kyando (9) aliyekuwa mkazi wa Mtaa wa Igoma ‘A’, Kata ya Isanga jijini Mbeya kusahaulika chumbani.

Alisema tukio hilo ambalo wakazi wa mtaa huo na Jiji la Mbeya walikumbwa na sintofahamu baada ya kujikuta wakizika jeneza tupu katika kaburi lililotarajiwa kuzikwa mwili wa marehemu huyo ambao baadaye iligundulika uliachwa ndani ya chumba alichohifadhiwa kwenye nyumba ya wazazi wake, lilitokea Januari 16.

Ilivyokuwa tukio lenyewe.

Tukio hilo lilisababisha kusambaa kwa taarifa nyingi tofauti zikiwamo zilizodai “mtoto amefufuka” huku wengine wakisema “ni maajabu ya mwisho wa dunia”.

Akisimulia kisa hicho, mwenyekiti wa mtaa huo, Fredy Mwaiswelo alisema baada ya kifo cha mtoto Kyando msiba uliendeshwa na taratibu za mazishi zilifanyika huku jeneza lilipelekwa msibani na kuwekwa chumbani kando ya mwili wake ambao ulikuwa umeviringishwa kwa blanketi na kulazwa chini kwenye godoro.

Alisema kuwa baadaye waombolezaji walichukuliwa jeneza hilo kwenda nalo makaburini na kulizika.

Mwaiswelo alisema waombolezaji waliporudi nyumbani walitaharuki baada ya kuambiwa na mwili wa marehemu uko chumbani umelazwa eneo ulipokuwa awali.

Alisema kutokana na hali ya taharuki iliyowakuta waombolezaji hao walitoa taarifa polisi ambao walifika na kurejesha hali ya amani kwa kuuchukua mwili wa marehemu na kwenda kuuhifadhi Hospitali ya Rufaa Mbeya.

“Mwili haukuagwa kama ilivyozoeleka ambapo marehemu anapotolewa ndani huwekwa nje na kila mtu anatoa heshima zake, badala yake mwili ulivyotoka ndani ukabebwa moja kwa moja kuelekea makaburini kwa ajili ya mazishi,” alisema mwenyekiti huyo.

Alisema baada ya kukamilisha waombelezaji walirudi nyumbani kwa wazazi wa marehemu kwa ajili ya shughuli nyingine na wakiwa hapo, ghafla mama ambaye hakumtaja jina alitoka ndani na kuwataka watu kutolia kwa kuwa marehemu yupo ndani amelala kwenye godoro.

Mwaiswelo alisema baada ya taarifa hiyo ilitokea taharuki ambayo ilisababisha watu kujiuliza maswali mengi bila majibu.

Baba wa marehemu, Jailo Kyando (36) alipotakiwa kuelezea tukio hilo alisema hakujua kilichotokea hadi mwili wa mtoto wake ukasahahulika ndani na kuzikwa jeneza tupu kwa kuwa yeye hakuhusika kumuandaa marehemu hadi kumweka kwenye jeneza, bali zilifanywa na ndugu zake.

“Kwa kweli sielewi chochote, kwani mimi sikushughulika na taratibu za kumuandaa mwanangu, hivyo sijui kilichotokea, lakini mwanangu alikuwa anasumbuliwa na kifafa kwa muda mrefu na leo tulipoamka asubuhi tumekuta amefariki (dunia),” alisema.

Mkazi wa eneo hilo, Beny Chikwanda ambaye ni rafiki wa baba wa marehemu alisema wao kama waombolezaji ilikuwa vigumu kujua kama ndani ya jeneza kuna mwili wa marehemu ama la.

Alisema mwili huo haukuagwa hadharani na kilichofanyika ni kuutoa ndani kisha kuubeba moja kwa moja kwenda makaburini.

“Hili jambo limetuacha bumbuazi na tunajiuliza maswali bila kupata majibu inakuwaje mtu aliyezikwa akaonekana ndani?” alihoji Chikwanda.

Haikufahamika mapema kama tukio hilo lilisababishwa na uzembe au bahati mbaya kwa wafiwa kusahau kuweka mwili wa marehemu kwenye jeneza ama kulikuwa na hujuma zozote.

Hata hivyo, Kamanda Mpinga alisema mwili huo baadaye ulizikwa upya kwa kufuata taratibu.

Mama kufukua kaburi

Mpinga alisema tukio la pili ni la mama mzazi aliyetambulika kwa jina la Ruth Segeti (57), mkazi wa Pipeline nje ya Jiji la Mbeya kushirikiana na watu wengine kufukua kaburi la mtoto wake kisha kuuchukua mwili wa marehemu kwenda kuuhifadhi nyumbani kwake akiwa na imani kwamba atafufuka.

Kamanda Mpinga alisema tukio hilo lilitokea Februari 18 ikiwa ni siku mbili tangu marehemu azikwe kifo kilichotokana na kisukari.

Mpinga alisema mwili wa marehemu baadaye ulizikwa upya Februari 20 kwa usimamizi na Halmashauri ya Wilaya Mbeya Vijijini.

Kuungua soko la Sido.

Agosti, 2017 Jiji la Mbeya lilikumbwa na simanzi nyingine baada ya wafanyabiasha wa soko la Sido lililopo Mwanjelwa kuunguliwa mali zao kutokana na moto uliozuka ndani ya soko hilo.

Moto huo ambao ulidaiwa kuanzia katika moja ya vibanda vya soko ulianza saa tatu usiku ambapo pamoja na jitihada za kuokoa mali, ilishindana, hivyo kuteketea zote. Baada ya tukio hilo, uongozi wa wilaya na mkoa uliunda kamati maalumu ya uchunguzi iliyoongozwa na katibu tawala Wilaya ya Mbeya, Hassan Mkwawa na katika mkutano wa hadhara uliofanyika wiki moja baadaye alisema ilibaini kwamba chanzo cha moto huo ni matumizi ya jiko la mkaa.

Pia, Mkwawa alisema kamati yake ilijiridhisha kwamba hasara iliyotokana na tukio hilo ni Sh14.293 bilioni kwa mali zote za wafanyabiashara hao ambazo ziliteketea. Baada ya tukio hilo wafanyabiashara hao waliiomba Serikali kuwaruhusu kujenga vibanda vya kudumu ili kuepusha majanga ya moto ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara kwenye masoko ya jijini hapa.

Ombi hilo lilikubaliwa na Serikali, ambapo Septemba 10, mkuu wa mkoa, Amos Makalla aliwataka wafanyabiashara hao kuendelea na ujenzi wa vibanda vya kudumu kwa kutumia matofali.

Katibu wa wafanyabiashara wa soko hilo, Alanus Ngogo aliushukuru uongozi wa Serikali. Tayari wafanyabiashara wengi walishaanza biashara zao ndani ya soko hilo baada ya kukamilisha ujenzi wao.

-->