Polisi watoa notisi vigogo waliotajwa na Magufuli kukamatwa

Kamanda wa polisi mkoa wa Mara Juma Ndaki

Muktasari:

Vigogo wanaotakiwa kukamatwa ni mfanyabiashara Mauza Nyakirang’anyi, Otieno Igogo na Gideon Mazara ambao wanadaiwa kukaidi wito wa Takukuru.

Musoma.  Jeshi la polisi mkoani Mara limetoa notisi ya kukamatwa kwa mfanyabiashara Mauza Nyakirang’anyi akidaiwa kushindwa kuripoti ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Mara kama alivyotakiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa mapema wiki hii.
Pia polisi mkoani Mara inachunguza alipo mfanyabiashara Otieno Igogo ambaye pia hajaripoti kama alivyotakiwa baada ya kutoa taarifa kuwa yupo nchini China kwa matibabu wakati simu yake ya mkononi ikionyesha yupo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo Septemba 14, Kamanda wa polisi mkoa wa Mara Juma Ndaki amesema tayari ofisi yake imeshawasiliana na Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera kwa ajili ya  kumkamata Nyakirang'anyi ambaye anadaiwa kukaidi wito wa kamati ya ulinzi na  usalama huku akidaiwa kuwa yupo mjini Bukoba mkoani Kagera.

Mwanzoni mwa wiki hii mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima amesema katika kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Rais John Magufuli aliyoyatoa wakati akiwa ziarani mkoani Mara wiki iliyopita, kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Mara iliwataka Nyakirang'anyi, Igogo pamoja na Dk Gideon Mazara kuripoti Takukuru kwa mahojiano.

Wanatuhumiwa kumiliki na uharibifu wa mali za umma ikiwamo Hoteli ya Musoma na kiwanda cha maziwa Utegi.

"Tayari nimeshatoa oda ili Mauza akamatwe popote alipo huku tukiendelea kuchunguza alipo Igogo maana mitambo yetu mpaka asubuhi ya leo ilikuwa inaonyesha simu yake ipo Dar sasa tunataka tujiridhishe kama kweli yupo China au amejificha,"amesema Ndaki.
Kamanda Ndaki amesema mtuhumiwa Mazara ameshindwa kufika kwa mahojiano baada ya wakili wake kutoa taarifa kuwa  yupo nchini Uingereza kwa ajili ya matibabu ya mke wake.
Watu hao walitakiwa kuripoti ofisi za Takukuru kabla ya Septemba 13 saa 8 mchana na hadi sasa hakuna aliyeripoti.
Hata hivyo Igogo tayari amesharejesha hati ya shamba la Utegi lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 10,000 serikalini toka Agosti 15 mwaka huu huku Nyakirang'anyi naye akirejesha hati ya umiliki wa Hoteli ya Musoma serikalini toka Septemba 11 mwaka huu.