Wawili wauawa kwa kupigwa risasi na polisi

Muktasari:

  • Kamanda Mambosasa ametoa onyo kwa wanaojihusisha na uhalifu, akisema wamejipanga kuwashughulikia.

Dar es Salaam. Watu wawili wanaodaiwa kuwa majambazi wameuawa kwa kupigwa risasi na Polisi, mmoja akituhumiwa kuwa alihusika katika tukio la kuvamiwa na kujeruhiwa Meja Jenerali mstaafu Vincent Mritaba.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema tukio hilo limetokea jana Jumatano saa nne usiku eneo la Mbezi Mshikamano kwa Mgalula.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi, Kamanda Mambosasa amesema mtuhumiwa anayehusishwa na kumjeruhiwa Meja Jenerali mstaafu Mritaba pia aliwahi kufungwa.

"Ametumikia adhabu ya kifungo mara kadhaa na alipotoka aliendelea na shughuli zake na jana ndiyo ilikuwa mwisho wake," amesema.

Kamanda Mambosasa akizungumzia tukio la kuuawa kwa watuhumiwa hao, amesema awali wakiwa kwenye pikipiki walifika eneo la tukio na kuuliza ni wapi wanapoweza kupata huduma ya fedha kwa njia ya mtandao.

Amesema mkazi wa eneo hilo ambaye ni mmiliki wa duka aliwatilia shaka hivyo alipiga simu kwa mkuu wa upelelezi.

Kutokana na taarifa hiyo, amesema askari waliokuwa doria walifika eneo hilo ambako waliwakuta watu watatu waliokuwa wamejificha mbali kidogo na duka la huduma ya M-pesa.

Kamanda Mambosasa amesema baada ya kuwaona polisi, watu hao walikimbia huku wakirusha risasi kujihami na kuwashambulia askari.

Amesema polisi walipambana nao na kuwajeruhi wawili ambao walifariki dunia wakipelekwa Hospitali ya Mwananyamala.

Kamanda Mambosasa amesema katika tukio hilo, polisi walikamata bunduki aina ya SMG iliyokuwa na risasi tisa na maganda mawili ya risasi.

Amesema uchunguzi unaendelea eneo la Mbezi. Pia, ametoa rai kwa watu wanaojihusisha na uhalifu kuacha akisema wamejipanga kupambana nao.

“Watu wote wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu, Dar es Salaam sasa si mahali salama kwa kuwa Jeshi la Polisi limejipanga kupambana na wahalifu wote,” amesema.