Possi asema kuajiriwa si suluhisho la changamoto

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge na Vijana), Dk. Abdallah Possi.

Muktasari:

Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge na Vijana, Dk. Abdallah Possi kwenye maadhimisho ya siku ya kujitolea kimataifa iliyoadhimishwa jijini hapa leo.

Dar es Salaam. Vijana nchini wametakiwa kufanya kazi za kujitolea ili kuisaidia jamii kutatua changamoto mbalimbali pia kuepukana na kilio cha kukosa ajira kutokana na kukosa ujuzi wa kazi.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge na Vijana, Dk. Abdallah Possi kwenye maadhimisho ya siku ya kujitolea kimataifa iliyoadhimishwa jijini hapa leo.
Possi amesema kuajiriwa si kigezo pekee cha watu kutatua changamoto mbalimbali katika jamii ila kuna fursa kubwa katika kujitolea inayowezaa saidia jamii.
"Kuna faida nyingi katika kujitolea kwanza ni jamii inayokuzunguka na nchi kwa ujumla kupata ufumbuzi na msaada wa matatizo pili ni uzoefu hasa pale unapopata elimu na hujapata ajira na hujui ni mbinu gani za kufanya," amesema Possi
Siku ya kufanya kazi kwa  kujitolea duniani huadhimishwa katika mataifa 193 duniani yaliyomo ndani ya Umoja wa Mataifa na lengo kuu ni kuwashawishi vijana wengi duniani kufanya kazi za kujitolea.