Profesa Kikula sasa asimulia milima na mabonde ya Udom

Muktasari:

  • Ataka Mwalimu Nyerere kuenziwa kwa vitendo
  • Profesa Kikula alitoa kauli hiyo wiki iliyopita wakati wa maadhimisho ya miaka 10 ya Udom yaliyokwenda sanjari na kumbukumbu ya miaka 18 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Ataka Mwalimu Nyerere Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Profesa Idrisa Kikula amesema ujenzi wa chuo hicho haukuwa katika ilani ya uchaguzi ya CCM, bali lilitokana na wazo la haraka la Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.

Profesa Kikula alitoa kauli hiyo wiki iliyopita wakati wa maadhimisho ya miaka 10 ya Udom yaliyokwenda sanjari na kumbukumbu ya miaka 18 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Alisema kumekuwa na kauli kuwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2005/10 ilikuwa na wazo la kujengwa Udom jambo ambalo si kweli bali kilichoandikwa katika ilani hiyo lilikuwa ni wazo la kuongeza udahili kwa wanafunzi katika vyuo vikuu vilivyokuwapo.

“Hili ni wazo binafsi la Jakaya Kikwete wakati huo akiwa Rais, tulifika hapa Februari 5, 2007 na kukutana na pori huku mifuko ikiwa mitupu,” alisema Profesa Kikula.

Makamu mkuu huyo wa Udom, alisema kazi ya kuijenga Udom haikuwa lelemama na ilifanywa kwa kutumia fedha za Watanzania kupitia mifuko ya hifadhi ya jamii ya LAPF, PPF na NSSF.

Kuhusu Mwalimu Nyerere, Profesa Kikula alisema kiongozi huyo hakuwa wa mfano na hawezi kulinganishwa kwa sasa na mtu mwingine, kwa kuwa busara zake zinatosha kuonyesha uzalendo aliokuwa nao.

Alitaka kuenzi kwa vitendo, fikra na harakati za kiongozi huyo katika kudhibiti vitendo vya ubadhirifu, rushwa na uzalendo katika kuleta maendeleo nchini.

Profesa Kikula alisema hawezi kumsahau Mwalimu Nyerere kutokana na kumtabiria kuwa atakuja kuwa kiongozi walipokutana mara ya kwanza 1976.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maadhimisho ya Miaka 10 ya Udom, Profesa Julius Nyahongo alisema chuo hicho kinatambua umuhimu wa Mwalimu Nyerere katika kupigania maslahi ya Taifa, kusimamia maadili na uzalendo kwa viongozi na watawala.