Profesa Mbarawa alivyohitimisha mjadala wa ATCL

Muktasari:

Pia, alitoa majibu juu ya tofauti ya utengaji fedha za ujenzi wa barabara kati ya Wakala wa Barabara (Tanroads) na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura).

Fidelis Butahe, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa jana alitumia dakika 35 kujibu hoja za wabunge kuhusu utendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Pia, alitoa majibu juu ya tofauti ya utengaji fedha za ujenzi wa barabara kati ya Wakala wa Barabara (Tanroads) na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura).

Awali, wabunge walitoa hoja mbalimbali walipochangia mjadala wa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2018/2019.

Profesa Mbarawa alibainisha kuwa, ATCL haijafanyiwa ukaguzi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) tangu mwaka 2007 hadi 2014/2015.

Kukodi ndege

Akizungumzia hoja za wabunge waliotaka Serikali ikodishe ndege badala ya kununua alisema, “Kununua ndege mpya ni jambo zuri kama zinatumika kwa muda mrefu. Kampuni nyingi za ndege kwa mfano, Kenya Airways zote zinanunua ndege mpya, wanakodi ndege kwa sababu maalumu,”alisema.

“Kununua ndege mpya unapata faida kwa sababu punguzo ni kubwa na inakupa faida katika uendeshaji kwa sababu mpya gharama zake za matengenezo ni ndogo ikilinganishwa na iliyozeeka.”

Akifafanua, alisema kuna kukodi ndege ikiwa na marubani na bila marubani. “Njia rahisi ni kukodi ndege bila marubani. Bei ya wastani wa kukodi ndege kwa mwezi ni Dola 200,000 (za Marekani ambazo ni zaidi ya Sh480 milioni hadi (Dola) 250,000 za Marekani (zaidi ya Sh550 milioni).”

“Gharama za matengenezo kwa mwezi ni Dola 18,000 za Marekani (zaidi ya Sh40 milioni). Ukikodi ndege unatakiwa kulipa Dola 25,000 (zaidi ya Sh60 milioni) kwa mwezi kama kodi TRA. Kwa mwezi mmoja angalau uwe na Dola 300,000 (zaidi ya Sh600 milioni); kwa mwaka ni Dola 3.5 milioni (zaidi ya Sh7.5 bilioni). Ukichukua na bima unatakiwa uwe na Dola 4 milioni (zaidi ya Sh10 bilioni). Ndege za Air Tanzania kipindi cha kuishi ni miaka 35, kipindi hicho chote ukikodi utatumia Dola 140 milioni (zaidi ya Sh260 bilioni), lakini sisi tunanunua ndege moja kwa Dola 35 milioni (zaidi ya Sh80 bilioni.”

“Kukodi ndege ni gharama kubwa kuliko kununua. Sasa hapo ipi faida, ukanunue au ukakodi? Eeh! wabunge nawauliza?” Alihoji Profesa Mbarawa na kujibiwa na baadhi ya wabunge wengi, “tununue.”

Alisema Rwanda ina ndege nane na zote imenunua akibainisha hata wabunge wanapokwenda bungeni hufikiria kununua nyumba kwa sababu kukodi ni gharama.

Ununuzi wa ndege kwa kampuni tofauti

Profesa Mbarawa akizungumzia ununuzi wa ndege kutoka kampuni tofauti kwamba utaongeza gharama za matengenezo, alisema Serikali inanunua itakayoleta faida kwa shirika na Watanzania.

“Unapotaka kununua ndege lazima uangalie ukubwa wa viwanja vyenu. Huwezi kupeleka ndege aina ya Jet katika uwanja wa ndege wa Tabora. Lazima ununue ndege kutokana na hali ya hewa ya nchi yako, pia lazima uangalie mwinuko wa kiwanja cha ndege kule unakokwenda,” alisema.

“Mfano, unataka kwenda Mumbai, India lazima utafute ndege itakayokupa faida ukienda Mumbai. Mfano Shirika la Ndege la Ethiopia wana Airbus, Boeing na Bombardier wakija Dar es Salaam inakuja Bombardier maana ndiyo inafaa zaidi kuja Dar es Salaam.”

ATCL kuondolewa IATA

Kuhusu ATCL kuondolewa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Ndege (IATA) kwa sababu ya madeni alisema ni kweli liliondolewa mwaka 2008 na kwa sasa Serikali inajipanga kulirejesha na kabla ya mwaka huu kumalizika litaingia tena katika mfumo huo.

ATCL kutokaguliwa

Pia alijibu hoja ya ATCL kutokaguliwa na CAG na hesabu zake kutowasilishwa bungeni.

“Serikali katika jitihada zake za kufufua ATCL ilibaini hesabu zake zilikuwa hazijakaguliwa tangu mwaka 2007 hadi mwaka 2015. Serikali tulimuagiza CAG kufanya ukaguzi wa hesabu za shirika katika kipindi hicho chote,” alisema.

“Kazi hiyo imekamilika na ripoti imepelekwa kwenye bodi ya ATCL, sasa tunafanya ukaguzi wa mwaka 2015/16 na 2016/17. Lengo ni kuhakikisha shirika linasimama. Tunataka kila fedha tutakayoweka itumike sawasawa.”

Mpango wa biashara

Huku akionyesha mpango wa biashara kwa wabunge, Profesa Mbarawa alisema shirika hilo linao na hubadilishwa kila mara kutokana na mahitaji ya soko, Watanzania na wateja.

“Ndege za ATCL zinafanya safari Dar es Salaam, Dodoma, Kigoma, Tabora, Mwanza, Bukoba, Kilimanjaro, Zanzibar, Songwe na Comoro. Hivi karibuni tutaanza safari za kwenda Mpanda, Tanga, Uganda na Burundi. Kumekuwa na ongezeko la mapato ghafi kutoka Sh34.4 bilioni mpaka Sh43.8 bilioni,” alisema.

Kuhusu Tarura

Akiizungumzia Tarura alisema, “Mfuko wa fedha za barabara unagharamia miradi ya barabara kuu na barabara za mikoa ambazo zinasimamiwa na Tanroads na za wilaya zinazosimamiwa na Tarura. Tanroads na Tarura zinatoa fedha katika mfuko huu lakini kuna vigezo.”

“Kwanza tunaangalia urefu wa mtandao wa barabara, kigezo cha pili tunaangalia barabara kama ni lami, changarawe au udongo, kigezo kingine tunaangalia wastani na uzito wa magari yanayopita,” alisema.