Putin ataka kuachana na matumizi ya dola

Muktasari:

  • Akilihutubia Bunge baada ya kuapishwa Jumatatu kuongoza muhula wa nne, Putin alitoa wito wa “kupunguza mzigo” wa uchumi wa Urusi kutokana na hatari ya kutawaliwa na sarafu ya Marekani.

Moscow, Urusi. Kuanzia muhula huu wa utawala wake Rais Vladimir Putin ameelezea moja ya malengo yake kuwa ni kuachana na matumizi ya sarafu ya dola ya Marekani katika uchumi wa Urusi akisema ni hatari kuiacha ihodhi soko la fedha.
Tangazo hilo limekuja katika kipindi ambacho Urusi na China zinajaribu kuboresha mkataba wa mauziano ya mafuta na ushirikiano wa fedha.
Akilihutubia Bunge baada ya kuapishwa Jumatatu kuongoza muhula wa nne, Putin alitoa wito wa “kupunguza mzigo” wa uchumi wa Urusi kutokana na hatari ya kutawaliwa na sarafu ya Marekani katika manunuzi ya mafuta kutoka soko la bidhaa kimataifa. Mkuu huyo wa zamani wa shirika la ujasusi la Urusi, KGB, alidokeza kwamba sababu kubwa zinahusiana na masuala ya usalama.
“Tulikuwa wanyofu, lakini sasa tunaona kwamba sheria za Shirika la Biashara Duniani (WTO) mara nyingi huvunjika, vikwazo vinawekwa kwa sababu za kisiasa, ambazo huita vikwazo. Pamoja na hayo vikwazo huwekwa ili kupata faida zake za upendeleo kiushindani,” alisema Putin.
Alisema kwamba “vikwazo” vipya vinavyovunja kanuni za biashara ya kimataifa vinaifanya dunia ione kwamba dola ya Marekani kuhodhi soko ni hatari kwa maeneo mengi. Kwa mujibu wa Putin kuachana na matumizi ya dola lazima kufanyike kwa kanuni ili kulinda utaifa wa nchi.
Hata hivyo, Putin hakutaja sarafu mbadala katika hotuba yake. Sarafu ya Urusi inaitwa ruble na ile ya China ni yuan iliyozinduliwa hivi karibuni katika biashara ya mafuta.