Putin arejea Ikulu kwa kishindo

Muktasari:

Apata ushindi wa asilimia 76 ukiwa mkubwa zaidi ya miaka iliyopita, huku upinzani ukilalamikia faulo. Kutokana na ushindi huo sasa atakaa madarakani hadi 2024.ata chini ya asilimia moja.

 


Moscow, Urusi. Rais Vladimir Putin Jumapili alipata ushindi mnono katika uchaguzi mkuu wa rais uliompa kipindi kingine cha miaka sita kukaa madarakani kwa awamu ya nne huku uhusiano na nchi za Magharibi ukizidi kuzorota.

Putin, ambaye ameitawala Russia kwa karibu miongo miwili, alipata ushindi wa asilimia 76 ukiwa mkubwa zaidi ya miaka iliyopita, huku upinzani ukilalamikia faulo. Kutokana na ushindi huo sasa atakaa madarakani hadi 2024.

Waangalizi waliripoti vifaa vya kuwekea kura na matukio mengine ya udanganyifu wakati Ikulu ya rais, Kremlin, iliwahamasisha watu wengi kujitokeza ili kumhalalisha Putin kuongoza kipindi kingine cha nne.

Watu milioni 107 walikuwa na haki ya kupiga kura na kwa mujibu wa Tume Kuu ya Uchaguzi waliopiga kura walikuwa asilimia 60.

Takwimu za Tume zinaonyesha kwamba baada ya asilimia 90 kuhesabiwa, Putin alikuwa mbele kwa asilimia 76.4 akimwacha nyuma mpinzani wake wa Chama cha Kikomunisti, Pavel Grudinin akiambulia asilimia 12 ya kura.

Mwanasiasa mpigania uzalendo, Vladimir Zhirinovsky alifuatia akiwa na asilimia sita wakati mtangazaji wa zamani wa runinga, Ksenia Sobchak aliambulia asilimia 1.5 na wagombea wengine walipata chini ya asilimia moja.