Mahakama yaelezwa puto la Sethi limeisha muda, Rugemalira hana saratani

Muktasari:

Mahakama yataka madaktari wao waitwe

Dar es Salaam.Upande wa Mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi, utakatishaji fedha  na kuisababisha Serikali hasara, inayomkabili Mmiliki wa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL, Habinder Sethi na mfanyabiashara, James Rugemalira, umedai kuwa mshtakiwa Rugemalila hana saratani na puto la Sethi limeisha muda wake.

Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai ameeleza  hay oleo Ijumaa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati akitoa taarifa baada ya kwenda gerezani kama alivyotakiwa na Mahakama.

Swai meeleza mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuwa yeye alikwenda magereza kufuatilia hali za washitakiwa hao kama Mahakama ilivyoagiza.

Swai amesema washitakiwa hao wameomba magereza kuwa wakati wanapofanyiwa uchunguzi kiafya madaktari wao kutoka nje ya nchi wawepo.

"Sethi ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi hii, yeye anayeishi na puto tumboni tangu Desemba mwaka jana na limeisha muda wake na kwamba daktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili walimfanyia uchunguzi na kubaini kuwa puto hilo linatakiwa kuondolewa na mshtakiwa alishirikishwa katika hatua hiyo akaomba daktari wake kutoka Afrika Kusini awepo wakati wa kufanyiwa upasuaji na kuomba muda wa kuwasiliana na daktari huyo," ameeleza Swai.

Hata hivyo, Swai ameeleza kuwa madaktari wa hapa nchini wapo tayari kuondoa puto hilo kama afya ya mshtakiwa itaendelea kuathirika au kuwa mbaya.

Ameeleza kuwa kwa upande wa mshitakiwa wa pili (Rugemalira) yeye  anatibiwa na magereza pamoja na daktari wake anayeitwa Fred ambaye anachukua vipimo na kupeleka hospitalini kwake Sanitas na kurudisha majibu magereza.

Amedai katika majibu hayo yanaonyesha kuwa hana saratani kama alivyodai na kwamba Serikali inafuatilia afya zao kwani hakuna jambo nyeti litakaloweza kuhatarisha maisha yao.

Baada ya maelezo ya upande  wa mashtaka, washtakiwa hao waliomba madaktari wao kutoka India na Afrika Kusini kuwepo wakati wakifanyiwa uchunguzi wa kiafya.

Awali, wakili wa Sethi,  Alex Balomi  alidai kuwa wamethibitisha kuwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili haina uwezo wa kumfanyia upasuaji wa ama kuondoa au kuweka hilo puto kwa mteja wake hivyo kitu muhimu ni  madaktari wa Afrika Kusini kuwepo nchini na hili ni suala la kutilia mkazo.

 

"Sisi tumepokea maoni kutoka kwa hao madaktari wa Afrika Kusini  kuwa ni lazima wawepo wakati wa upasuaji wa Sethi," amesema wakili wa utetezi, Balomi.

Kwa upande wake, wakili wa Rugemarila, Respicious Didas ameeleza kuwa suala la afya ya washtakiwa ni muhimu sana na ugonjwa wa mteja wake upo wazi kwamba ana uvimbe unaoonekana.

"Licha ya ugonjwa wa mteja wangu kuwa wazi, bado upande wa mashtaka haujachukua hatua yoyote kuhusiana na uvimbe huo," ameeleza wakili Didas.

Amedai kuwa Rugemalira aliwahi kuugua saratani na kufanyiwa upasuaji mwaka 2008 na kwamba ugunduzi huo pamoja na matibabu yote, vilifanyika nchini India.

Didas alieleza kuwa matibabu na vipimo vikivyokuwa vinafanyika hapa nchini vilikuwa vina shida na ndio maana aliamua kuanzisha kituo cha saratani hapa kwa ajili kutibu wananchi wasio na uwezo wa kwenda kutibiwa nje ya nchi, wanaweza kupata matibabu katika kituo chake.

Wakili huyo alieleza kuwa anaamini kuwa mteja wake akitibiwa nchini India kulipo na vifaa vya kutosha wanaweza kugundua tatizo la uvimbe aliokuwa nao.

"Suala la afya ya mteja wangu linapaswa kupewa kipaumbele na ugunduzi wa ugonjwa wake ufanyike kwa kutumia madaktari wa India.”

Kutokana na maelezo ya mawakili wa utetezi, Hakimu Simba alisema Mahakama inashukuru kwa kuona kuwa amri iliyotoa Januari 5, mwaka huu ya washtakiwa hao wakatibiwe imetekelezwa.

Hakimu Simba alisema kutokana na hali hiyo, Mahakama imenukuu na imeona mshtakiwa wa kwanza wakati wa upasuaji, madaktari wake wa Afrika Kusini wawepo na utaratibu huo huo utumike kwa mshtakiwa wa pili.

"Magereza wawasiliane na madaktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili madaktari ya India wawepo wakati wa upasuaji," amesema Hakimu Simba.

Hata hivyo, Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 2, mwaka huu itakapotajwa.