Puto tumboni lamtesa bilionea Sethi wa IPTL

Muktasari:

  • Alisema hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Kisutu, Huruma Shaidi na kubainisha kuwa awali, Mahakama ilitoa amri mshtakiwa huyo apelekwe Muhimbili na kwamba baada ya kuwasiliana na mteja wao walibaini kuwa Magereza walimpeleka Hospitali ya Amana badala ya Muhimbili kinyume cha amri ya Mahakama.

Wakili Joseph Makandege ameomba Mahakama itoe amri mshtakiwa Harbinder Singh Sethi akatibiwe katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa sababu amewekewa puto (balloon) tumboni ambalo lisipopata huduma stahiki linaweza kupasuka na kumsababishia kifo.

Alisema hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Kisutu, Huruma Shaidi na kubainisha kuwa awali, Mahakama ilitoa amri mshtakiwa huyo apelekwe Muhimbili na kwamba baada ya kuwasiliana na mteja wao walibaini kuwa Magereza walimpeleka Hospitali ya Amana badala ya Muhimbili kinyume cha amri ya Mahakama.

Alisema Kifungu cha 53(1) cha Sheria ya Magereza Tanzania kinatoa fursa kwa mtu yeyote aliyewekwa ndani, mfungwa au mahabusi akiwa mgonjwa ana haki ya kupelekwa katika hospitali ya Serikali kwa matibabu.

Aliongeza kuwa hospitali iliyoelekezwa na Mahakama ni Muhimbili na siyo nyingine.

“Mahakama yako haikumung’unya maneno apelekwe Muhimbili, wao wakampeleka Amana ni rai yetu kuwa amri ya Mahakama haijatekelezwa hadi leo,” alisema na kuomba iagize amri hiyo itekelezwe.

Makandege alieleza kuwa amri ya hakimu kwamba mshtakiwa apelekwe Muhimbili ilikusudiwa ili kuhakikisha afya ya mshtakiwa inazingatiwa, inahifadhiwa ili hatimaye aweze kuhudhuria kwenye mashtaka yake.

Alibainisha kuwa hatua ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuamuru mshtakiwa huyo apelekwe Muhimbili ni baada ya kuzingatia kuwa mshtakiwa ana upasuaji ambao ulisababisha kuwekewa puto (balloon) kwenye tumbo lake.

Alisema kwa mujibu wa taarifa za kitabibu, mshtakiwa huyo asipohudumiwa ipasavyo, hali hiyo inaweza kumsababishia kifo.

Alisisitiza mshtakiwa apelekwe katika Hospitali ya Muhimbili kwa sababu ndiyo ya juu ya Serikali nchini ambayo inategemewa kwa kuwa na wataalamu na vifaa stahiki vya tatizo linalomkabili mteja wake.

Aliongeza kuwa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na inaongozwa na utawala wa sheria na kuelezea kushangazwa kwake iwapo imefikia hatua taasisi ya Serikali inaweza ikasigina amri za Mahakama na chombo hicho kisiwe na la kufanya akidai upande wa mashtaka unakaidi amri za mahakama na kwamba hiyo ni dharau kwa kuwa ndiyo kimbilio la wanyonge.

Hivyo aliiomba Mahakama itoe amri rasmi mshtakiwa Sethi apelekwe Muhimbili kupatiwa matibabu.

Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali Mkuu, Vitalis Peter alidai hakuna amri yoyote ya Mahakama ambayo upande wa mashtaka umeisigina, “Ni kweli Kifungu cha 53 (1) kinaipa mamlaka Magereza kumpeleka mtu aliye chini yao ambaye anaumwa hospitali, lakini wana utaratibu wao wa ndani, hospitali na wataalamu wao.”

Alisema Magereza ndiyo wanakaa nao kwa mara ya kwanza, wao ndiyo wanamuangalia mgonjwa, wakiona rufaa hospitali ya juu yao wanampa ndiyo sababu Sethi alipelekwa Amana.

Alieleza kuwa mbali ya Amana, Magereza walimpeleka Sethi kwa Dk Wilson kutoka Muhimbili ili amuangalie.

Kwa maelezo hayo, alihoji madai ya wakili Makandege kwamba Magereza haijatekeleza amri ya Mahakama na kumshauri awasiliane na mteja wake amueleze jinsi jeshi hilo lilivyojitahidi ili apate huduma za kiwango.

Kuhusu kumpeleka Amana, wakili Peter alidai kuwa Magereza hawachaguliwi na mtu pa kumpeleka mgonjwa, bali wataalamu wao ndiyo wanaochunguza na kuamua.

Pamoja na maelezo ya wakili Peter, Hakimu Shaidi alisisitiza na kuamuru Sethi apelekwe Muhimbili.

Kilio cha Rugemalira

Sethi na mwenzake James Rugemalira wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi yakiwamo matano ya kutakatisha fedha.

Jana, Rugemalira alilalamika kuwa licha ya kuwa na mawakili zaidi ya 10, Magereza hawampatii nafasi ya kuwaona wote.

Alidai kuwa kati ya mawakili hao ni wawili tu, waliopewa kibali cha kumuona hivyo kuiomba Mahakama apate nafasi ya kuonana nao kwa sababu ana mambo mengi ambayo kwa sasa hajui yanaendaje.

Hakimu Shaidi aliwaagiza maofisa wa Magereza walipokee hilo na kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 14 kwa kuwa upelelezi haujakamilika.