RC Luhumbi ataka madini yawanufaishe wananchi

Muktasari:

Akifungua kongamano la wadau wa madini lililohudhuriwa na wachimbaji wadogo kutoka mikoa yote, Luhumbi alisema bila wananchi kuhisi na kuona faida ya madini kupatikana kwenye maeneo yao, wachimbaji na wafanyabiashara hawawezi kufanya shughuli zao kwa amani.

Geita. Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Luhumbi amewataka wawekezaji na wafanyabiashara kuhakikisha maisha ya wananchi wanaoishi karibu na migodi yanaendana na utajiri unaopatikana katika maeneo yao.

Akifungua kongamano la wadau wa madini lililohudhuriwa na wachimbaji wadogo kutoka mikoa yote, Luhumbi alisema bila wananchi kuhisi na kuona faida ya madini kupatikana kwenye maeneo yao, wachimbaji na wafanyabiashara hawawezi kufanya shughuli zao kwa amani.

“Rasilimali ya madini inapaswa kuwa baraka badala ya laana kwa wananchi wanaoishi karibu na migodi,” alisema Luhumbi.

Mkutano huo umeandaliwa na Haki Madini kwa kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa ya Mazingira (IIED), Kituo cha Kimataifa cha Utafiti wa Misitu (CIFOR) na Kampuni ya Ushauri ya MTL.

Akizungumzia lengo la mkutano huo, mkurugenzi wa asasi isiyo ya kiserikali ya Haki Madini, Amani Mhinda alisema ni kuwawezesha wachimbaji kujadili na kutafutia ufumbuzi changamoto zinazoikabili sekta ya madini.

Mchimbaji wa madini wa kutoka Kampuni ya Nsangano Gold Mine, Renatus Nsangano alishauri pafanyike utafiti unaoonyesha maeneo yenye madini na kiwango kinachopatikana ili kuwaondolea wachimbaji adha ya kupoteza rasilimali fedha na muda kwa kuchimba eneo lisilo na madini.