Friday, August 10, 2018

RC Mbeya akomaa na uenyekiti CCM

 

By Godfrey Kahango, Mwananchi gkahango@mwananchi.co.tz

Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amesema hatajiuzulu uenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, bali atafanya kazi akiongozwa na misingi ya sheria.

Alisema hayo jana alipozungumza na viongozi wa dini katika ukumbi wa Mkapa jijini Mbeya.

Chalamila aliteuliwa hivi karibuni na Rais John Magufuli pamoja na viongozi wengine wa mikoa na wilaya.

Chalamila anafuata nyayo za Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi aliyeteuliwa na Rais John Magufuli mwaka 2016 kuwa mkuu wa mkoa huo huku akiwa pia ni mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya. Hata hivyo, katika uchaguzi wa chama hicho mwaka jana, Zambi hakutetea uenyekiti wake.

Chalamila alisema alianza kupata shinikizo la kujiuzulu kutokana na utaratibu mpya wa CCM wa mtu mmoja kuwa na cheo kimoja.

‘‘Nilipoteuliwa ukuu wa Mkoa wa Mbeya, mtu mmoja akasema sasa natakiwa kujiuzulu uenyekiti. Nikasema sijiuzulu kwa vile Rais ameniteua kuwa mkuu wa mkoa huku akijua mimi ni mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa. Ila nitajiuzulu kwa maelekezo ya Rais aliyeniteua ukuu wa mkoa,” alisema.

Akizungumza na Mwananchi baada ya mkutano huo, Chalamila alisema ukuu wa mkoa hausababishi shughuli za chama hicho mkoani Iringa kusimama.

Alisema kwa sasa anayekaimu uenyekiti ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na yeye atahudhuria vikao ambavyo hufanyika kila baada ya miezi mitatu.

Chalamila alisema kushika nyadhifa hizo mbili hakutamfanya awe na ubaguzi, bali ataongoza kwa kufuata sheria, kanuni na utaratibu hivyo hatakuwa na sababu ya kumuonea mtu.

“Mkuu wa mkoa ni mjumbe wa kamati ya siasa ya mkoa (CCM), lakini vilevile siasa ni imani ya mtu. Cha msingi isimdhuru mtu mwingine yeyote, hivyo sitamuonea mtu kwa misingi ya kisiasa, nitashirikiana na viongozi na wananchi wote bila ya ubaguzi,” alisema.

Mbali ya Chalamila na Zambi kushika ukuu wa mkoa wakiwa wenyeviti wa CCM wa mikoa, pia mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku ‘Musukuma’ alikuwa mwenyekiti wa chama hicho mkoani Geita huku akiwa mbunge. Hata hivyo kama ilivyo kwa wakuu hao wa mikoa hakutetea tena nafasi hiyo katika uchaguzi wa mwaka jana.

Maendeleo Mbeya

Chalamila alisema Mbeya ina hadhi ya kuitwa jiji, lakini miundombinu haiendani na uhalisia kutokana na mambo mengi ikiwamo siasa.

“Nimekuwa nikijiuliza, kweli Serikali imeshindwa kujenga barabara nne katikati ya jiji hili? Hivi kweli Serikali imeshindwa kujenga barabara ya kilomita 40 ya kuzungumza kuanzia Inyala hadi Mbalizi ili malori yapite huko? Kweli Serikali imeshindwa kuimarisha na kuufanya uwanja wa ndege kuwa na hadhi inayotakiwa?” alihoji Chalamila.

Aliwaomba viongozi wa dini kuwaelimisha vijana kutojikita katika ushabiki wa kisiasa na wawafundishe ujasiriamali.

Viongozi wa dini

Askofu wa Kanisa la Pentekoste Mkoa wa Mbeya, Nkumbu Mwalyego alisema jiji hilo halina mpangilio mzuri wa makazi kutokana na Serikali kutokuwa na mkakati wa kuliboresha.

Sheikh Hassan Katanga alisema ni muda mwafaka kwa jamii kutoa elimu kwa vijana ili waweze kujishughulisha na ujasiriamali.

-->