Monday, January 8, 2018

RC Mghwira: K’njaro tulielemewa na wageni Krismasi, Mwaka mpya

 

By Daniel Mjema, Mwananchi dmjema@mwananchi.co.tz

Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Anna Mghwira amesena kipindi cha sikukuu za Krismasi na Mwaka mpya, walipokea wageni na hakuona mahali popote kama vyuma vimekaza.

Mghwira alisema alitembelea baa na kumbi za starehe na kushuhudia watu wakinywa pombe hadi saa 11 alfajiri hali inayoashiria kwamba vyuma vilikuwa ni laini kabisa.

Mkuu wa mkoa alitoa kauli hiyo mjini Moshi jana katika misa ya shukrani kwa ajili ya mchungaji kiongozi wa Usharika wa Karanga wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Fred Njama.

Ibada hiyo iliyokuwa mahususi kwa Mchungaji Njama kutimiza miaka 30 tangu abarikiwe kuwa mchungaji, iliendeshwa na msaidizi wa Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT, Elingaya Saria.

Pia, ibada hiyo ilimhusisha Mchungaji Abinael Lema aliyewahi kuwa mchungaji kiongozi wa Usharika wa Karanga waliyebarikiwa kuwa wachungaji siku moja na Njama, kabla ya kustaafu.

Akizungumza katika ibada hiyo, alisema miaka ya nyuma uchumi wa Tanzania uliendesha kwa fedha haramu zikiwamo zilizotokana na dawa za kulevya, rushwa na ufisadi.

Alitolea mfano wa Mkoa wa Kilimanjaro unaopakana na nchi ya Kenya, akisema baadhi ya wafanyabiashara walikuwa wanaingiza bidhaa kutoka nje ya nchi bila kulipa kodi halali za Serikali.

“Kulikuwa na fedha ambazo hazikuwapo kwenye mfumo rasmi. Kwa hiyo ukiziba hii mianya lazima uchumi utatikisika. Ile pesa iliyokuwa inapatikana kirahisi haipatikani tena.”

Mchungaji Njama alimshukuru Mungu kwa kumpa nguvu na uwezo wa kulihubiri neno lake kwa miaka 30.     

-->