RC Mjini Magharibi awaonya wanaouza pombe Ramadhan

Muktasari:

Aagiza masheha kuhakikisha maeneo yao biashara hiyo haiendelei kufanywa

Zanzibar. Mkuu wa Mkoa Mjini Magharib Unguja, Ayoub Mohamed Mahmoud amesema hawatamvumilia yeyote anayejihusisha na biashara ya pombe katika mfungo wa Ramadhan.

Ayoub aliyasema hayo wakati akizungumza na gazeti hili lilipotaka kufahamu namna Serikali ya mkoa huo ilivyojipanga kukabiliana na biashara hiyo kipindi hiki.

Alieleza kuwa hatakuwa tayari kuona mtu anakaidi amri hiyo na kwamba, anayetaka ajaribu ili aone ukali wa sheria.

“Ni lazima kila mtu aheshimu na kutii sheria ikiwamo kufuata maagizo ya viongozi, Serikali hatutakuwa tayari kuona mtu mmoja au wawili wanaivuruga hali ya amani na utulivu kwa kuamua kuuza ulevi kipindi hiki, wakati walio wengi wanaendelea na funga,’’ alisema.

Licha ya hayo, Ayoub alisema waliwaagiza masheha wa shehia zote kufuatilia kwenye maeneo yao na wahakikishe hakuna biashara ya pombe inayofanyika.

Pia, Ayoub aliwataka wananchi kutoa ushirikiao watakapobaini kuwapo baadhi ya watu kwa namna moja au nyingine wanaoshiriki katika vitendo visivyofaa kwenye jamii.

Wakingumzia amri hiyo kwa nyakati tofauti juzi, baadhi ya wananchi walisema amri imekuja wakati mwafaka.

Mize Said wa Kiembesamaki alisema ingawa kilichoamriwa na Serikali ni sahihi, ila kutamka na kutekeleza ni vitu viwili tofauti.

Naye Jane Silima wa Kisauni aliwataka watumiaji pombe kuwa wavumilivu kipindi hiki, kwani mila na desturi za Zanzibar zinafahamika, ni lazima wawaheshimu wanaoendelea na ibada ya funga.