RC Mongella awapongeza wananchi, wavuvi wa Ukara

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amewapongeza wananchi na wavuvi wa Ukawa kwa kujitolea vifaa na ujuzi wao kuwaokoa waathirika wa Kivuko cha MV Nyerere

Ukara. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amewamwagia sifa wananchi, wakazi na wavuvi wa Kisiwa cha Ukara kwa kujitolea kufanya kazi ya uokoaji tangu ajali ya Kivuko cha Mv Nyerere kilipopinduka Septemba 20,2018.

Akitoa salaam za mkoa kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, leo Septemba 23, 2018 Mongella amesema wananchi wa kisiwa hicho walioanza kazi hiyo mara kivuko kilipopinduka na  hadi timu ya mkoa ulipowasili saa 10:45 alasiri, tayari watu 40 walikuwa wameokolewa.

"Wavuvi wa Kijiji cha Bwisya na kisiwa kizima cha Ukara wamejitolea bure boti zao za uvuvi wakipeana zamu kuopoa maiti. Ni vigumu kumshukuru mtu mmoja mmoja. Lakini Serikali ya mkoa inamshukuru kila mtu kwa nafasi yake," amesema Mongella.