RC Tanga kuhamasisha halmashauri kusaidia mahakama

Muktasari:

Asema  lengo ni kuyarejesha majengo ya mahakama katika ubora 

Tanga. Mkuu wa Mkoa wa  Tanga, Martin Shigella amesema atazihamasiha Halmashauri za Wilaya kuanza kutenga fedha kwa ajili ya kusaidia kutatua changamoto zinazokabili mahakama, ikiwemo uchakavu wa majengo.

Shigela ametoa kauli hiyo jana Januari 26, mwaka 2017  wakati akizindua maadhimisho ya wiki ya sheria nchini yanayofanyika katika viwanja vya mahakama kuu jijini hapa.

Shigella amesema ipo haja ya Halmashauri za Wilaya, Miji na Jiji kusaidia changamoto zilizoko kwenye mahakama katika maeneo yake.

Ametolea mfano mahakama za mwanzo, kwamba baadhi majengo yake yamechakaa kutokana na kujengwa miaka mingi iliyopita, hivyo kuhitaji ukarabati ili kuyarejesha katika ubora.

“Hatuwezi kujiita ni serikali za mitaa wakati mahakama ambazo zinafanya kazi  kwenye maeneo yetu zinakabiliwa na changamoto nyingi,” amesema Shigella.

Jaji mfawidhi wa mahakama kuu kanda ya Tanga, Imani Aboud amesema mahakama itahakikisha inatekeleza kwa vitendo matumizi ya Tehama.

“Tutaitumia wiki ya maadhimisho ya sheria kutoa

elimu  kwa wananchi ya namna  tunavyotoa huduma ya sheria, utoaji haki kabla na wakati wa kusikiliza mashauri mbalimbali,” amesema.