RC aagiza ukaguzi fedha zinazolipwa na mgodi

Muktasari:

Agizo hilo alilitoa baada ya kupokea malalamiko ya wananchi wa Mtaa wa Mgusu waliodai juzi kuwa GGM hutoa fedha kila mwezi kutokana na kazi zinazofanywa na vijana wa mtaa huo ndani ya mgodi, lakini hawajui mapato na matumizi ya fedha hizo.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel ameiagiza Halmashauri ya Geita kufanya ukaguzi ili kujua kama fedha ambazo Kata ya Mgusu inapewa na Mgodi wa Dhahabu Geita (GGM), zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Agizo hilo alilitoa baada ya kupokea malalamiko ya wananchi wa Mtaa wa Mgusu waliodai juzi kuwa GGM hutoa fedha kila mwezi kutokana na kazi zinazofanywa na vijana wa mtaa huo ndani ya mgodi, lakini hawajui mapato na matumizi ya fedha hizo.

Gabriel aliagiza uchunguzi ufanyike ndani ya siku saba na endapo itabainika kuna ubadhirifu viongozi husika wakamatwe na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Leornad Bugomola alisema kata ya hiyo ni miongoni mwa zile zinazopata fedha kila mwezi kutoka GGM, lakini malipo hayo hayafanyi kazi yoyopte ya maendeleo.

“Mheshimiwa mkuu wa mkoa kata hii ndiyo inayopokea fedha nyingi kutoka kwa wawekezaji, hii ni kata iliyopo karibu kabisa na mgodi lakini hatuoni kazi zinazofanywa na fedha hizo tatizo ni watendaji, naomba hili uingilie kati,” alisema Bugomola

Awali, diwani wa kata hiyo, Pastory Ruhusa alisema haina shule ya sekondari jambo ambalo hulazimu wanafunzi kutembea zaidi ya kilomita 20 kwenda shule za kata nyingine.

Alisema kutokana na tatizo hilo, baadhi ya wanafunzi huacha shule na kuingia kwenye shughuli za uchimbaji dhahabu zinazofanyika katika maeneo mbalimbali wilayani hapa.

“Ili mwanafunzi aende shule kila siku anahitaji nauli ya Sh3,000, kwa mzazi ni fedha nyingi na ukisema atembee kwa mguu anafika shuleni kachelewa na kurudi anafika usiku,” alisema Ruhusa.

Alisema kata hiyo yenye wakazi zaidi ya 20,000 haina zahanati wala kituo cha afya, jambo linalowalazimu wagonjwa kufuata huduma katika hospitali ya mkoa ambayo iko mbali.

Mkazi wa Mgusu, Anatoly Chale alisema kuna tatizo katika uongozi wa eneo hilo unaowalazimu kuishi maisha magumu licha ya kwamba dhahabu inachimbwa katika kata yao na kumtaka mkuu wa mkoa kuwasaidia.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, ofisa uhusiano wa jamii wa GGM, Manase Ndoroma alisema mgodi huo umekuwa ukichukua vijana kwenye mitaa na vijiji vinavyouzunguka ambao hulipwa Sh300,000, na kati ya fedha hizo Sh60,000 hurudi kwenye ofisi za vijiji kwa shughuli za maendeleo.